Mwakilishi wa TPA, Nchini Burundi Bw. Emmanuel Mrutu akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais wa Burundi, Mhe. Prosper Bazombanza mara baada ya kutembelea Bandala TPA katika maonyesho ya “EAC Regional Tourism Expo (EARTE’22)” yaliyofanyika mjini Bujumbura, Burundi

 

By Leonard Magomba

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeshiriki katika maonyesho ya kitalii ya Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama “EAC Regional Tourism Expo (EARTE’22)” na kutumia fursa hiyo kunadi Bandari zake.

Mbali na kunadi ufanisi wa Bandari zake, TPA pia ilitumia maonyesho hayo ya kitalii kuujulisha umma jinsi inavyokusudia kuboresha miundombinu ya kuhudumia meli za kitalii zinazotia nanga katika bandari zake, hususani Bandari Kuu ya Dar es Salaam.

Kivutio kikubwa katika maonyesho hayo kwa upande wa TPA ni jinsi Bandari yake ya Dar es Salaam inavyoweza kuhudumia meli za kitalii maarufu kama “Cruise Ships”.

Katika siku zijazo TPA inafikiria kujenga gati maalum katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuhudumia meli za kitalii zinazofika pwani ya Afrika Mashariki. Hatua hiyo itapanua wigo wa huduma zinazotolewa na TPA nje ya huduma za shehena zinazotoka na kuingia nchini.

Maonyesho ya EARTE’22 yalifanyika mjini Bujumbura kuanzia tarehe 23 hadi 30 Septemba, 2022.

Akizungumza na Waandishi wa Habari hapa mjini Bujumbura, Mratibu wa maonyesho hayo kwa upande wa Tanzania, Dkt. Glastone Mlay alisema maonyesho hayo yalikuwa ni fursa kwa Tanzania kujitangaza na kutangaza vivutio adhimu vya utalii vinavyopatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi.

“Tumefanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa taasisi za Tanzania zinashiriki katika maonyesho haya kwa mafanikio ili kutangaza vivutio vyetu na namna tunavyoweza kuwahudumia watalii wetu kwa ubora zaidi,” amesema.

Jumla ya taasisi 84 zimeshiriki katika maonyesho kutoka katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwa upande wa Tanzania kuna jumla ya Taasisi 20 pamoja na watu binafsi walioshiriki katika maonyesho haya, alisema Dk.Mlay.

Dk. Mlay alisema kwamba film ya Royal Tour, na Maonyesho ya Kimataifa ya Kiswahili maarufu kama “Swahili International Tourism Expo” na Utalii Meli za Kitaalii maarufu kama “Cruise Ship Tourism” ni miongoni mwa vitu vilivyovutia zaidi katika maonyesho hayo.

Mwisho