Na Leonard Magomba

Jumla ya Wafanyakazi 265 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wamenufaika na mafunzo maalumu ya maandalizi ya kustaafu.

Mafunzo hayo yanayotolewa na TPA kwa kushirikiana na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yamelenga kuwandaa watumishi hao na maisha ya baadae baada ya kustaafu, amesema Bi. Concepter Kadula, wakati anafungua rasmi mafunzo hayo.

“Menejimenti imeandaa mafunzo ya maandalizi ya kustaafu kwa watumishi wetu wapatao 265 ambao wametimiza umri wa kustaafu kuanzia miaka 55 na kuendelea,” amesema Bi. Concepter Kadula.

Bi. Kadula ambaye alifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TPA alisema kwamba lengo la mafunzo haya ni kuwawezesha wastaafu watarajiwa waweze kujiandaa kwa kuweka mipango wezeshi ili kuyamudu maisha ya baadae baada ya kustaafu.

Aidha, alisema kwamba menejimenti ilifanya hivi baada ya kubaini kuwa watumishi wengi huingiwa na hofu pindi muda wa kumaliza utumishi wao unapokaribia.

“Hii hofu inatokana na kutojiandaa vema kimaisha kwa kuwekeza katika miradi midogo midogo ambayo itasaidia katika kuingiza kipato na kuweza kumudu maisha ya kila siku baada ya kustaafu.

Menejimenti imeona ni vema kupata mafunzo haya ili yawaweke sawa kisaikolojia kwa kuwa na mtazamo chanya juu ya kuyaendea maisha mapya baada ya kustaafu utumishi wa umma.

Kwa mujibu wa mratibu wa mafunzo hayo kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma, Bw. Felicianus Richard amesema katika mafunzo hayo watatoa elimu kuhusu mipango na mikakati ya kustaafu, elimu ya Afya na utunzaji wa fedha, mtindo bora wa maisha na ujasiriamali.

Elimu nyingine iliyotolewa katika mafunzo hayo yaliyofanyika Bagamoyo ni pamoja na jinsi ya kuanzisha miradi inafaa na kutembelea miradi mbalimbali na kuona namna ya uanzishwaji na uendeshwaji wake ili tuweze kujifunza.

Mwisho