Na Leonard Magomba
Jumla ya Wafanyakazi 265 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wamenufaika na mafunzo maalumu ya maandalizi ya kustaafu.
Mafunzo hayo yanayotolewa na TPA kwa kushirikiana na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yamelenga kuwandaa watumishi hao na maisha ya baadae baada ya kustaafu, amesema Bi. Concepter Kadula, wakati anafungua rasmi mafunzo hayo.
“Menejimenti imeandaa mafunzo ya maandalizi ya kustaafu kwa watumishi wetu wapatao 265 ambao wametimiza umri wa kustaafu kuanzia miaka 55 na kuendelea,” amesema Bi. Concepter Kadula.
Bi. Kadula ambaye alifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TPA alisema kwamba lengo la mafunzo haya ni kuwawezesha wastaafu watarajiwa waweze kujiandaa kwa kuweka mipango wezeshi ili kuyamudu maisha ya baadae baada ya kustaafu.
Aidha, alisema kwamba menejimenti ilifanya hivi baada ya kubaini kuwa watumishi wengi huingiwa na hofu pindi muda wa kumaliza utumishi wao unapokaribia.
“Hii hofu inatokana na kutojiandaa vema kimaisha kwa kuwekeza katika miradi midogo midogo ambayo itasaidia katika kuingiza kipato na kuweza kumudu maisha ya kila siku baada ya kustaafu.
Menejimenti imeona ni vema kupata mafunzo haya ili yawaweke sawa kisaikolojia kwa kuwa na mtazamo chanya juu ya kuyaendea maisha mapya baada ya kustaafu utumishi wa umma.
Kwa mujibu wa mratibu wa mafunzo hayo kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma, Bw. Felicianus Richard amesema katika mafunzo hayo watatoa elimu kuhusu mipango na mikakati ya kustaafu, elimu ya Afya na utunzaji wa fedha, mtindo bora wa maisha na ujasiriamali.
Elimu nyingine iliyotolewa katika mafunzo hayo yaliyofanyika Bagamoyo ni pamoja na jinsi ya kuanzisha miradi inafaa na kutembelea miradi mbalimbali na kuona namna ya uanzishwaji na uendeshwaji wake ili tuweze kujifunza.
Mwisho
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa akijibu hoja mbalimbali toka Kamati ya Bunge ya Miundombinu mjini Dodoma
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavara akifafanua jambo wakati akijibu hoja mbalimbali toka Kamati ya Bunge ya Miundombinu mjini Dodoma
Mkurugenzi Mpya wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Mrisho S. Mrisho
Na Levina Msia
Mkurugenzi Mpya wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Mrisho S. Mrisho amefungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Bandari ya Dar ea Salaam na kubainisha vipaumbele vyake ili kuongeza ufanisi.
Katika kikao hicho ambacho ni cha kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi ya Ukurugenzi wa Bandari hiyo, Mkurugenzi huyo alibainisha vipaumbele vyake vinavyolenga kuongeza ufanisi katika utendaji bandarini hapo.
Miongoni mwa vipaumbele alivyoainisha kuvisimamia kwa haraka ni pamoja na kuongeza kasi ya upatikanaji wa vitendea kazi, uboreshaji wa maeneo ya utendaji kazi, kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya ofisi na maeneo mbalimbali ya shughuli za utekelezaji.
vingine ni pamoja na kuisafisha Bandari kwa kupanga vyema yadi za kuhifadhia shehena, kuvuka malengo ya kiutendaji, kutoa motisha kwa wafanyakazi wanaofanya vizuri, kuimarisha kitengo cha ‘welfare’ ili kukabiliana na matatizo ya ndani ya wafanyakazi, kusimamia kwa karibu michakato ya manunuzi kwa lengo la kufanikisha upatikanaji wa mahitaji muhimu kama vile vipuri na uboreshaji wa Viwanja vya Michezo.
Wajumbe wa Baraza wameahidi kumpatia ushirikiano Mkurugenzi wa Bandari na kumhakikishia kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya Taasisi na Serikali kwa ujumla.
Mwisho
Na Leonard Magomba
Wafanyabiashara toka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), wamefanya ziara ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam ili kujionea miundombinu ya Bandari hiyo pamoja na kukagua maboresho mbalimbali yaliyokwishafanyika na yanayoendelea kufanyika.
DRC ambalo ndilo soko kuu kwa Bandari ya Dar es Salaam hutumia Bandari hiyo kupitisha bidhaa mbalimbali haswa za madini ya aina mbalimbali yanayopatikana nchini humo, sambamba na mazao ya misitu.
Kwa upande wa bidhaa zinazoingia kutoka katika soko la kimataifa, DRC inapitisha bidhaa za nafaka, magari, mitambo, mavazi, vinywaji, mafuta na bidhaa za chuma.
Kabla ya ziara ya kutembelea miundombinu ya Bandari, wafanyabiashara hao walifanya mazungumzo katika ukumbi wa mikutano uliopo jingo la TPA Tower na menejimenti ya TPA chini ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Lufunyo Hussein.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Lufunyo aliwakaribisha na kuwashukuru kwa kuendelea kuiamini na kutumia Bandari za TPA hususani Dar es Salaam, Tanga na Kigoma kupitisha shehena mbalimbali zinazoingia na kutoka nchini DRC.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu alitumia fursa hiyo, kuwahakikishia usalama wa mizigo yao na utayari wa TPA kuendelea kutoa huduma bora na zenye ufanisi zaidi kwa wafanyabiashara hao kwa maslahi mapana ya nchi zote mbili.
Akifafanua kuhusu Ulinzi na Usalama, Dkt. Lufunyo aliwaeleza wafanyabiashara hao jinsi mifumo ya kisasa ya Ulinzi na Usalama inavyofanyakazi ambapo alisema TPA imefunga takribani Kamera 400 za CCTV kuzunguka eneo la Bandari nzima ambazo zinafanyakazi saa 24.
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe wa wafanyabiashara hao kutoka nchini DRC katika miji ya Kalemie, Uvira, Bukavu na Goma, Mwenyekiti wa Umoja huo aliishukuru TPA kwa huduma bora zinazotolewa katika Bandari hiyo.
Mwenyekiti huyo alisema kwamba, kwasasa mizigo yao inahudumiwa kwa ufanisi na kuwafikia kwa wakati.
Pia alipongeza kuwa siku 30 huru zinazotolewa na TPA kwa wafanyabiashara wa DRC pasipo kutozwa tozo ya kuhifadhia mizigo (storage charges) imesaidia wafanyabiashara hao wa DRC wanaotumia Bandari hizo kupunguza gharama za kupitisha Shehena kwenda katika miji hiyo.
Mwenyekiti huyo, aliwahakikishia TPA kuwa wafanyabishara hao toka nchini DRC wapo tayari kuendelea kufanyabishara na Bandari za TPA kwani zimekuwa na unafuu mkubwa wa gharama na wenye faida mtambuka kwa pande zote ukilinganisha na Bandari shindani.
mwisho