Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko amewataka wadau wa Ushoroba wa Kati kutumia fursa zilizopo ili kupunguza gharama za kufanya biashara.

Kakoko amesema ni jukumu la wadau wa usafirishaji kujipanga vizuri ili kuokoa muda wa safari na kutoa huduma bora katika usafirishaji wa mizigo ya wateja kwa kuondoa vikwazo mbalimbali. Akitoa mfano alisema, kuna shehena ya tani takriban milioni 40 mpaka 50 katika Ushoroba wa Kati ambayo wadau wanashindwa kutumia fursa kuihudumia badala yake ni tani milioni 16.2 tu ambazo zinapita katika Ushoroba huo.

“Changamoto nyingi zinatokana na wadau kutotumia vizuri fursa zilizopo katika shoroba zetu haswa hii ya Kati katika kupunguza gharama za biashara,” amesema.

Mhandisi Kakoko ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa warsha ya Kimataifa iliyoandaliwa na Kamati ya Serikali ya Kudumu ya Usafirishaji (Inter Governmental Standing Committee on Shipping- ISCOS) iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo ambayo imeundwa na nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Zambia inaendesha warsha ya siku mbili ambayo imekutanisha wadau wa usafirishaji kujadili masuala mbalimbali yatakayohusu usafiri wa majini na nchi kavu kwa kaulimbiu isemayo “International Freight Logistics Best Practices.

Akizungumzia kuhusu mikakati ya TPA kama lango la biashara nchini, Kakoko amesema asilimia 90 ya biashara ya Kimataifa hapa nchini inapitia katika bandari na hivyo TPA imejipanga kuwekeza katika miundombinu na vifaa vya kisasa, kuendeleza rasilimali watu, kuongeza na kuboresha matumizi ya TEHAMA, kuendeleza juhudi za kimasoko ili kumsogeza mteja karibu na kudumisha usalama wa mizigo katika bandari zote.

Warsha hii inaendelea kesho ambapo TPA itatoa mada itakayohusu jitihada zinazofanyika katika kuboresha huduma zinazotolewa na bandari ya Dar es Salaam.

DG KAKOKO

GROUP PHOTO

OUTSIDE