TPA YAENDELEA KUTOA FURSA ZA MAFUNZO KWA VITENDO KWA WANAFUNZI!
Wanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE) na wengine kutoka shule za Boabab, Kinzudi na Twiga za jijini Dar es Salaam wamefanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam ili kujifunza kwa vitendo namna Bandari ya Dar es Salaam inavyotoa huduma zake mbalimbali.
Afisa Msaidizi Utekelezaji, Bw. Denis Mapunda amesema ziara za wanafunzi ni muhimu ili kuongeza uelewa wa shughuli za Bandari miongoni mwa wadau mbalimbali.
Ameongeza kwamba mbali na ziara hizo pia Mamlaka inafanya jitihada kadhaa za kutumia vyombo vya habari kuelimisha wateja kuhusiana na suala la kushughulikia nyaraka za kutoa mzigo mapema kabla mzigo husika haujafika bandarini.
Wanafunzi hao wamehaidi kuwa mabalozi wazuri wa Bandari ya Dar es Salaam ili kuiwezesha Bandari hiyo kuongeza ufanisi katika kutoa huduma zake kwa wakati.
Katika ziara hiyo Wanafunzi hao walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Gati namba 1-5 (eneo ambalo meli zinafunga wakati wa kupakua au kupakia mizigo), kitengo cha kukagua mizigo “Scanners” na kitengo cha nafaka cha "Grain Terminal”.