Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeshiriki katika kampeni maalum ya Samia Nivike Kiatu iliyolenga kuwafikia watoto wenye shida ya viatu.

TPA imechangia Jumla ya Tshs 65.9 milioni kwa ajili ya ununuzi wa viatu vya watoto, fulana na gharama za usafiri kwa ajili ya kusambazia viatu hivyo kwa watoto wanaokwenda shule bila kuvaa viatu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bi. Beatrice Jairo amesema kwamba tunatambua kuwa kuna changamoto nyingi zinazoikabili jamii yetu na kwa kuwa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao imeona kuna umuhimu wa kuanzia zoezi hili Zanzibar (Unguja na Pemba) basi tunatoa Rai kwenu pia kuwa zoezi hili lisiishie huko tu bali lije na Tanzania bara.

Bi Jairo alisema kwamba tunaomba lije na huku Tanzania Bara ili nako muweze kuwavisha watoto wengine viatu. Samia Nivike Kiatu ni kampeni inayosimamiwa na Taasisi ya Wasanii ya Mama Ongea na Mwanao. Pia ametoa wito kwa taasisi nyingine nazo kuunga mkono Kampeni hiyo.

Alisema kuwa TPA inalo jukumu la kushiriki katika masuala yanayohusu jamii kupitia Sera yake ya Misaada kwa Jamii “Corporate Social Responsibility,” ambapo inashiriki kikamilifu kurudisha faida yake kwa jamii.

Kwenye Sera ya Misaada kwa Jamii, TPA imekuwa ikilitekeleza jukumu la kutoa misaada kwa kuhudumia jamii katika Sekta ya Elimu, Afya, Maendeleo ya Jamii pamoja na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza.

Katika kuhakikisha tunaunga mkono azma ya Serikali katika  kuhudumia jamii, lakini pia kujenga mahusiano mema na wateja, wadau na umma kwa ujumla, TPA iliona jambo hili ni jema na la kheri na kuona kuna haja ya kuwasaidia.

mwisho