Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mikeli Mbossa akiongea na Wahariri wa Vyombo vya habari mjini Bagamoyo.

 

Na Leonard Magomba

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mikeli Mbossa amekutana na Wahariri wa Vyombo vya habari mbalimbali kwa lengo la kufahamiana na kubadilishana mawazo.

Katika kikao hicho, Bw. Mbossa pia alitumia fursa hiyo kuelezea mipango mbalimbali ya Mamlaka haswa maboresho makubwa yaliyofanyika katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara pamoja na Bandari za Maziwa.

 

Wahariri hao pia walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali kuhusu TPA na shughuli zake na jinsi inavyohudumia masoko yake hususani katika nchi za Zambia, DRC, Rwanda, Burundi, Malawi, Uganda, Zimbabwe na Sudani ya Kusini.

TPA imefanya maboresho makubwa katika Bandari zake ili kuongeza ufanisi na kuhudumia wateja wake kwa ubora na haraka zaidi.

Katika maboresho hayo, bandari zilizofaidika ni pamoja na ya Dar es Salaam ambapo maeneo kadhaa yaliboreshwa; Moja ni ujenzi wa gati jipya na maalumu kwa ajili ya kuhudumia shehena ya magari, eneo lenye uwezo wa kuhifadhi magari takribani elfu sita (6,000) kwa wakati mmoja.

Kuchimba kina cha magati kutoka mita saba hadi 14.5, kutanua lango la kuingilia meli (Entrance channel), kupanua eneo la kugeuzia meli (Turning basin), pamoja na kuboreshwa kwa magati toka gati namba moja hadi saba.

Kwa Bandari ya Mtwara, imefanyiwa maboresho ya kujengwa gati Na. 2 lenye urefu wa mita 300, huku Bandari ya Tanga ikichimbwa kuongeza kina, kupanua lango la kuingizia meli, sambamba na kujengwa gati yenye urefu wa mita mia tatu (300) ili kuwezesha meli kubwa za mizigo kushusha makasha na mizigo mchanganyiko moja kwa moja gatini, tofauti na awali ambapo makasha na mizigo mingine ilikuwa ikishushwa nangani kisha kupakiwa kwenye meli ndogo zenye uwezo wa kutia nanga katika magati ya zamani yaliyokuwa na kina kifupi.

Kwa upande wa Bandari za Maziwa, TPA imejenga Bandari mpya na ya kisasa ya Karema iliyoko Wilayani Tanganyika, Mkoani Katavi, Bandari za Kabwe, Kassanga zilizo Ziwa Tanganyika na Bandari ya Ndumbi iliyopo Ziwa Nyasa.

Mwisho