Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imejipanga kujenga matenki ya kuhifadhi mafuta (Farm tanks) yenye uwezo wa kuhifadhi tani 360,000 kwa wakati mmoja.
Ujenzi wa matenki hayo ni mpango mkakati wa kuwezesha meli zinazokuja kupakua mafuta zisikae Bandarini muda mrefu na hivyo kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za ununuzi wa mafuta kwa mtumiaji wa mwisho.
Maendeleo hayo yalibainika wakati Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile alipofanya ziara yake ya kwanza ya kikazi katika Bandari ya Dar-es-Salaam tangia kuteuliwa kwake kama Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi.
Katika ziara yake, Mhe. Kihenzile ametembelea eneo litakalojengwa matenki hayo ya kuhifadhi mafuta, eneo la kuhifadhi mizigo inayoharibika (perishable goods), gati la Mafuta la Kurasini Oil Jetty (KOJ), Gati Na. 1-7, Gati la Magari RoRo na Gati la Meli za kwenda Zanzibar na Visiwa vya Comoro.
Baada ya ziara hiyo, Mhe. Naibu Waziri ameipongeza Menejimenti ya TPA na kuitaka kusimamia miradi hiyo ya kimkakati kikamilifu ili ikamilike kwa wakati na kuhakikisha thamani ya uwekezaji (value for money) inapatikana.
Mwisho