Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) itajenga gati mpya na ya kisasa yenye urefu wa mita 500 katika Bandari yake mama ya Dar es Salaam.
Ujenzi wa gati hiyo ambayo itakuwa ni gati namba 12-15 ni muendelezo wa mpango mkakati wa Serikali wa kuboresha miundombinu na huduma katika Bandari hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Bodi ya Shirika la Bandari Zanzibar, iliyongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Joseph Meza, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Mkurugenzi wa Mipango, Ubora na Vihatarishi, Dkt Boniphace Nobeji amesema kwasasa mpango huo upo katika hatua ya upembuzi yakinifu.
“Kwasasa tupo katika hatua ya kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa ujenzi wa gati mpya namba 12-15 katika Bandari ya DSM,” amesema Dkt Nobeji kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA.
Dkt Nobeji amsema kwamba gati hizo za kuhudumia Makasha zinakadiriwa kuongeza uwezo wa Bandari ya DSM kuhudumia Makasha kwa TEUs 2.5 milioni kwa mwaka, ifikapo mwaka 2047.
Mbali na ujenzi huo, TPA tayari imempata mkandarasi wa kujenga Gati na Matenki ya kuhifadhia mafuta katika Bandari hiyo.
“Kwa kuanzia kutajengwa gati na matenki 17 yenye uwezo wa kupokea na kuhifadhi mafuta hadi tani 362,500 kwa wakati mmoja,” amesema.
Kukamilika kwa mradi huu, amesema kutaongeza ufanisi wa Bandari ya DSM kuhudumia meli za mafuta na kupunguza gharama na changamoto zinazojitokeza kwa sasa za uchelewaji wa meli za mafuta.
Kupitia mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP), Serikali kupitia TPA imeshafanya maboresho ya gati namba 1-7 na gati maalumu la kuhudumia magari yaani RoRo.
Bandari ya DSM inahudumia takriban asilimia 90 ya soko lote la Tanzania ambapo kwa upande wa biashara ya kimataifa Bandari hii inahudumia asilimia 95 ya shehena yote ikilinganishwa na Bandari zote nchini.
Bandari ya DSM inahudumia nchi nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kama vile; Malawi, Zambia, DR Congo, Burundi, Rwanda na Uganda.
Hivi karibuni, nchi ya Sudani Kusini pia imeonesha nia ya kutumia Bandari ya DSM.
Kwa upande wa ukubwa wa soko, Bandari hii inahudumia eneo lenye takriban watu 700 milioni