Na Leonard Magomba

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekabidhi meli zake tatu kwa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) ili izisimamie na kuziendesha kwa ajili ya kutoa huduma za kusafirisha abiria na mizigo katika Ziwa Nyasa.

Meli hizo ambazo ni MV Njombe, MV Ruvuma na MV Mbeya II zilizokuwa zikimilikiwa na TPA, zilitengenezwa na Mamlaka kwa lengo la kusaidia kutoa huduma za kusafirisha abiria na mizigo katika mwambao wa Ziwa hilo.

 

 

Kati ya meli hizo tatu, mbili ni za mizigo na zina uwezo wa kubeba tani 1000 kila moja nay a abiria ina uwezo wa kubeba tani 200 na abiria 200 kwa wakati mmoja.

Mikoa inayonufaika na huduma za meli hizo ni pamoja na Ruvuma, Njombe na Mbeya huku nchi zitakazohudumiwa na meli hizo ni Malawi na Msumbiji.

Uwepo wa meli hizo umekuwa kichocheo kikubwa cha kukuza biashara kati ya mikoa hiyo mitatu na nchi jirani za Malawi na Msumbiji huku ikisaidia kwa kiwango kikubwa kutatua changamoto sugu za usafiri katika Ziwa hilo.

Katika makabidhiano hayo yaliyoshuhudiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce  Mbossa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini mstaafu, Inspekta Jenerali (IJP), Ernest Mangu pamoja na uongozi wa MSCL na TASAC.