BALOZI WA RANDWA NCHINI TANZANIA AMEFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM
Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Patrick Nyamvumba, tarehe 21 Mei 2026 alikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus Abed, katika ziara yake ya siku moja iliyolenga kujionea shughuli za uendeshaji wa bandari, kujifunza kuhusu mifumo ya usafirishaji na uhifadhi wa mizigo, pamoja na kujadili changamoto na fursa za kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Rwanda.Katika mazungumzo hayo, Balozi Nyamvumba ameipongeza Serikali ya Tanzania pamoja na TPA kwa maboresho makubwa ya miundombinu ya bandari na usafirishaji. Aidha, ameonesha matarajio makubwa kuhusu miradi inayoendelea kutekelezwa, ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Kuhifadhi Mafuta cha Liquid Bulk Terminal Kigamboni, matumizi ya Reli ya Kisasa (SGR), pamoja na ujenzi wa barabara zinazounganisha Tanzania na Rwanda, ambayo itasaidia kuongeza ufanisi wa biashara na usafirishaji wa mizigo kati ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus Abed, amesema kuwa kutokana na ongezeko la meli na shehena ya mizigo bandarini, Serikali kupitia TPA imechukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma. Hatua hizo ni pamoja na kuanza kwa ujenzi wa gati moja lenye urefu wa mita 500 katika eneo la Malindi, ujenzi wa gati kumi upande wa pili wa bandari, uboreshaji wa miundombinu ya barabara, pamoja na matumizi ya Reli ya Kisasa (SGR) na Reli ya MGR kuelekea Kwala ili kuharakisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini.Aidha, Bw. Abed ameeleza kuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya wateja kuchelewa kutoa mizigo yao bandarini kwa wakati, hali inayosababisha msongamano wa mizigo. Hivyo, amewataka wateja kuhakikisha wanatoa mizigo yao kwa wakati ili kutoa nafasi kwa bandari kuendelea kuhudumia shehena nyingine zinazoendelea kuwasili.Katika ziara hiyo, ujumbe wa Rwanda ulipata pia fursa ya kutembelea Kituo cha Kuhudumia Mafuta cha Kurasini Oil Jetty, ambapo ulijionea namna shehena ya mafuta inavyohudumiwa kuanzia kuwasili bandarini hadi kufikishwa kwa wateja.

EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"