Sélectionnez votre langue

Bandari ya Kilwa imeendelea kupokea na kuhudumia meli za Kitalii ambapo tarehe 15 Januari 2026 meli iitwayo MV ISLAND SKY imewasili ikiwa na jumla ya watalii 89 pamoja na wafanyakazi wa meli 79.

Watalii hao wanatoka nchi za Uingereza, Uholanzi, Ireland, Ujerumani, Finland na Australia ambao wamewasili katika Mji wa Kilwa kwa lengo la kutembelea vivutio mbalimbali vya asili vyenye kubeba historia kubwa ya Afrika Mashariki ambavyo vimekuwa vikitangazwa kwa nia ya kukuza Utalii katika Ukanda wa Kusini na Tanzania kwa ujumla.

Vilevile, Watalii hao wamepata fursa ya kujionea mradi mkubwa unaoendelea wa ujenzi wa Bandari ya Kisasa ya Uvuvi katika Bandari ya Kilwa. Wageni hao wamepongeza hatua hiyo na kusisitiza kuwa, kuongezeka kwa vivutio vya Utalii pamoja na miundombinu bora ya Bandari vitachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la idadi ya Watalii wanaotembelea eneo hilo siku kwa zijazo.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mkuu wa Idara ya Ubaharia Kapteni Paul Mchwampaka amesema, Bandari itaendelea kuhudumia meli za Utalii kwa ufanisi mkubwa ili kuendelea kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan za kukuza Sekta ya Utalii ambayo ni nguzo kubwa katika kuitangaza nchi na kuongeza pato la Taifa.