Sélectionnez votre langue

Bandari ya Mtwara imefanya kikao cha Wadau wa Bandari tarehe 11 Mei, 2026. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Klabu ya Bandari kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya maboresho ya huduma za kibandari.Akifungua kikao hicho, Meneja wa Bandari ya Mtwara Bw. Ferdinand S. Nyathi aliwaomba wadau wote kutoa maoni na mapendekezo juu ya changamoto wanazokutana nazo wakati wa kupata huduma Bandarini kwa lengo la kuweka mazingira bora zaidi ya 
utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika shughuli za kibandari

Katika majadiliano yaliyofanyika, wadau mbalimbali walitoa maoni na mapendekezo yaliyolenga kuboresha huduma za Bandari ikiwemo kuendelea kufanyika kwa mapitio ya Tariff mpya ili iendane zaidi na mazingira halisi ya biashara. 
Sambamba na maoni hayo, wadau walitoa pongezi kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania kutokana na maboresho makubwa ya miundombinu yanayoendelea kufanyika pamoja na kuimarika kwa huduma zinazotolewa katika Bandari ya Mtwara. Walieleza kuwa, kasi ya utoaji wa huduma imeongezeka, mazingira ya kazi yameboreshwa na ushirikiano kati ya watendaji wa Bandari na wadau umeendelea kuwa mzuri na wenye tija. 

Wadau hao pia walipongeza juhudi za uongozi wa Bandari katika kusikiliza maoni ya wadau mara kwa mara, jambo ambalo limeendelea kujenga mahusiano mazuri na kuongeza imani kwa wateja. Vilevile walieleza kuridhishwa na hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kuboresha usalama wa mizigo pamoja na kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara kupitia Bandari ya Mtwara. Akifunga kikao hicho, Meneja wa Bandari Bw. Ferdinand Nyathi aliwashukuru wadau kwa 
kuitikia wito wa kushiriki kikao hicho muhimu. Aidha, alielezea kupokea changamoto, maoni, mapendekezo na pongezi zilizowasilishwa na wadau na kuahidi kuzifanyia kazi kwa haraka ili kuendelea kuimarisha utolewaji wa huduma.
Aidha, alisisitiza kuwa Bandari ya Mtwara itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wake ili kuhakikisha huduma zinaendelea kuboreshwa na Bandari hiyo kuwa kitovu muhimu cha biashara na uchumi katika ukanda wa Kusini mwa  Tanzania na nchi jirani