Sélectionnez votre langue

Bandari ya Mtwara imeendelea kuonesha uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena ya magari, baada ya kupokea na kuhudumia meli nne zilizowasili ndani ya kipindi cha wiki moja na kushusha zaidi ya magari 1,500, hatua inayozidi kuimarisha nafasi ya bandari hiyo kama kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania na nchi jirani. Magari yaliyoshushwa bandarini hapo yanahusisha yale yanayobaki nchini kwa ajili ya matumizi ya soko la ndani pamoja na yanayosafirishwa kwenda katika nchi jirani, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia na Malawi kupitia Ushoroba wa Mtwara (Mtwara Corridor). Mafanikio hayo yanadhihirisha kuongezeka kwa imani ya wateja wa ndani na wa kimataifa katika kutumia Bandari ya Mtwara, ambayo imeendelea kuwa lango muhimu la biashara kwa nchi zinazotumia bandari za Tanzania kufikisha na kupokea mizigo yao.

Ongezeko la shughuli za ushushaji wa magari limechangiwa na maboresho makubwa yaliyofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya bandari, matumizi ya vitendea kazi vya kisasa, uwekezaji katika mifumo ya TEHAMA, punguzo la tozo mbalimbali pamoja na kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kuzingatia viwango vya ubora na weledi. Wakati huo huo, Bandari ya Mtwara inatarajia kupokea meli nyingine nne ndani ya wiki ijayo, ambazo zinatarajiwa kushusha zaidi ya magari 1,000. Matarajio hayo yanaashiria kuendelea kuongezeka kwa shughuli za biashara kupitia bandari hiyo na kuimarika kwa mchango wake katika kukuza biashara ya kikanda na uchumi wa taifa.
Kuendelea kuongezeka kwa idadi ya meli na shehena zinazohudumiwa katika Bandari ya Mtwara ni uthibitisho wa mafanikio ya uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali kupitia TPA katika kuboresha huduma za bandari, kwa lengo la kuongeza ushindani, kuvutia wateja zaidi na kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha huduma za usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini