BANDARI YA MTWARA YAPONGEZWA KWA MABORESHO YA MITA YA MAFUTA
Wataalam wa masuala ya nishati kutoka nchini Malawi wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika miundombinu ya kuhudumia shehena ya mafuta katika Bandari ya Mtwara, wakieleza kuwa hatua hiyo imeongeza ufanisi wa bandari na kuimarisha huduma za usafirishaji wa mafuta kwa nchi za ukanda huo. Pongezi hizo zimetolewa na timu ya wataalam 10 wa masuala ya nishati kutoka Malawi waliofanya ziara ya kikazi katika Bandari ya Mtwara tarehe 23 Julai, 2026, wakiongozwa na Mtaalam wa Masuala ya Udhibiti wa Uchumi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Malawi (Malawi Energy Regulatory Authority – MERA), Bw. Alex Calvin Banda. Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mnyororo mzima wa huduma za shehena ya mafuta katika Bandari ya Mtwara, kuanzia meli zinapowasili bandarini, upakuaji wa mafuta, uhifadhi wake katika matanki yanayomilikiwa na kampuni za sekta binafsi, hadi upakiaji katika malori yanayosafirisha mafuta kwenda katika nchi mbalimbali, ikiwemo Malawi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand Nyathi, alisema bandari imefanya maboresho makubwa ya miundombinu kwa kuongeza uwezo wa njia za kupokea na kusukuma mafuta kwenda kwenye matanki ya kuhifadhia, hatua ambayo imeongeza kasi na ufanisi wa utoaji wa huduma. Alifafanua kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya TPA na sekta binafsi, ambao umewezesha uwekezaji katika miundombinu ya kuhudumia shehena ya mafuta na hivyo kuongeza tija katika usafirishaji wa mafuta kwa soko la ndani na nchi jirani.
Kwa upande wao, wataalam hao walieleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa maboresho ya mfumo wa kupokea, kupima na kusukuma mafuta (Flow Meter), wakisema teknolojia hiyo imeongeza uwezo wa Bandari ya Mtwara kuhudumia shehena kubwa za mafuta kwa ufanisi zaidi. Aidha, walisisitiza kuwa Malawi itaendelea kuitumia Bandari ya Mtwara kama lango muhimu la kupitishia shehena ya mafuta kutokana na maboresho yaliyofanyika na ubora wa huduma zinazotolewa, jambo linaloimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Malawi.
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"