Sélectionnez votre langue

Kwa mara ya kwanza katika historia, Bandari ya Mtwara inatarajiwa kuanza kupokea mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa uchimbaji wa gesi asilia katika eneo la Nanguruwe, Mkoa wa Mtwara.

Hatua hiyo imebainika baada ya ugeni wa wafanyabiashara na viongozi wa Kampuni ya ARA Petroleum Tanzania kufanya ziara maalum katika Bandari ya Mtwara kwa lengo la kujiridhisha na uwezo wa bandari hiyo kuhudumia shehena kubwa za mitambo ya mradi huo kuanzia mwezi Agosti, 2026.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Meneja wa ARA Petroleum Tanzania, Bw. Hilal Al Hinai, amesema lengo la ziara hiyo lilikuwa kutathmini miundombinu, vitendea kazi pamoja na ufanisi wa bandari katika kushughulikia mizigo mizito na mikubwa.

Amefafanua kuwa kuanzia mwezi Agosti, 2026, kampuni hiyo inatarajia kuanza kupokea meli zitakazobeba vifaa vya mradi huo, ambapo kila meli itakuwa na zaidi ya tani 1,000 za mitambo na vifaa mbalimbali vitakavyotumika katika uchimbaji wa gesi eneo la Nanguruwe.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mkuu wa Idara ya Masoko, Bw. Faraji Mbulalina, amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wengi zaidi kutumia bandari hiyo, akieleza kuwa ina uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena mbalimbali kwa ufanisi.

Bw. Mbulalina amesema Bandari ya Mtwara imeendelea kuboreshwa na kwa sasa ina unafuu wa tozo za kibandari, miundombinu wezeshi, vitendea kazi vya kisasa pamoja na rasilimali watu wenye ujuzi na weredi wa hali ya juu, hivyo kuwa chaguo sahihi kwa miradi mikubwa ya kimkakati.

ARA Petroleum Tanzania ni kampuni ya uchimbaji na uzalishaji wa mafuta na gesi, inayojihusisha na maendeleo ya rasilimali za gesi asilia katika eneo la Ntorya – Mtwara Kusini. Kampuni hiyo ni tawi la ARA Petroleum yenye makao yake nchini Oman, iliyoanzishwa kusimamia na kuendeleza mradi wa gesi uliogunduliwa chini ya Ruvuma Production Sharing Agreement (PSA).