Sélectionnez votre langue

Bandari ya Tanga imeendelea kuwa chaguo sahihi kwa wafanyabiashara na wadau wa usafirishaji nchini baada ya kufanikiwa kupokea meli mbili za MV BBC WASHINGTON na MV ZI- JING- SONG zilizobeba mitambo mizito ya kisasa kwa ajili ya miradi mbalimbali inayoendelea nchini.

 

Meli hizo zimetia nanga katika bandari hiyo moja ikiwa imebeba mitambo ya kudhibiti umeme katika mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la kwenda Uganda (EACOP) na nyingine ikiwa imebeba mitambo ya kisasa ya kuzalisha umeme mali ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

 

Meneja wa Utekelezaji kutoka kampuni ya “East Africa Logisticts Services “ ambaye ndiye msimamizi wa mitambo hiyo Bw. Steve Miller amesema kuwa, mitambo hiyo 95 imeletwa na meli ya MV BBC WASHINGTON kutoka nchini Singapore na inatarajia kwenda Chongoleani Mkoani Tanga kwa ajili ya kudhibiti umeme katika bomba la mafuta kwenda Uganda la EACOP.

 

Naye wakala wa meli ya MV ZI-JING- SONG kutoka China Bw. Clinton Kitiku wa kampuni ya “Government Clearing Agent” (GPSA)  alisema kuwa, meli hiyo iliyokuwa imebeba mitambo 10 ya kufua umeme na matanki 80 ya kuhifadhi mafuta ambayo ni mali ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inatajiwa kwenda Mikoa ya Tunduma, Iringa na Mbeya.

 

Ujio wa meli hizo katika Bandari ya Tanga ni  baada ya uboreshaji wa miundombinu na uwepo wa vitendea kazi vya kisasa kuweza kuhudumia shehena na mizigo mizito  “Heavy lifting” imekuwa kivutio kwa wadau wa usafirishaji kutumia na kuiamini bandari hiyo katika utoaji wa huduma bora

.