Sélectionnez votre langue

Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Salehe Mbega ametoa rai kwa wadau wa usafirishaji wa bandari hiyo kukitumia Chama cha Madereva wa Masafa Marefu (CHAMATTA) Mkoa wa Tanga ambacho kwa sasa kinatambulika kihalali baada ya kupata vibali vyote kutoka mamlaka husika.

Bw. Mbega alitoa rai hiyo kwenye uzinduzi wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la “Bandari House”

Akiongea katika uzinduzi huo Bw. Mbega alisema kuwa, uwepo wa chama hicho katika Mkoa wa Tanga utasaidia kuibua fursa za ajira hususani madereva ambao ndio mhimili wa usafirishaji wa mizigo katika Bandari ya Tanga.

“Bandari ya Tanga imekuwa na ongezeko kubwa la shehena ya magari yanayoshuka  kwa wastani wa magari 1500 kwa mwezi ambapo asilimia 70 ni magari  yanayoenda nchi jirani “Transit” hivyo nawaasa madereva kutumia fursa ya ajira kupitia CHAMATTA “. Aliongeza Bw. Mbega

Katika hatua nyingine Bw. Mbega alikitaka chama hicho kusimamia maadili kwa madereva ili kujenga uaminifu na kuweka imani kwa wateja wanaopitisha mizigo Bandari ya Tanga.

Awali akitoa utambulisho kwa viongozi wa chama hicho, Mwenyekiti wa CHAMATTA Mkoa wa Tanga Bw. Adamu Mwenda alisema kuwa, kuanzishwa  kwa chama hicho Mkoa wa Tanga ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

Aidha Bw. Mwenda aliipongeza Bandari ya Tanga kwa ushirikiano na kuthamini mchango wa madereva wa masafa marefu “Transit” Mkoa wa Tanga hivyo alitoa wito kwa wadau wa usafirishaji kukitumia chama hicho.