BARAZA DOGO LA MAJADILIANO YA BANDARI LAFANYA KIKAO CHAKE CHA 73 MTWARA
Baraza Dogo la Majadiliano la Bandari ya Mtwara limefanya kikao chake cha 73 tarehe 13 Machi, 2026, kilichoongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Ferdinand S. Nyathi ambaye pia ni Meneja wa Bandari ya Mtwara.
Katika kikao hicho, wajumbe walipata fursa ya kujadili na kubainisha mafanikio na mwelekeo chanya unaoendelea kuonekana katika maendeleo ya Bandari ya Mtwara.
Katika majadiliano hayo imeelezwa kuwa, maboresho ya miundombinu ya Bandari yanaendelea kutekelezwa kwa lengo la kuongeza ufanisi wa shughuli za upakiaji na upakuaji wa mizigo. Maboresho hayo yanahusisha ukarabati wa maeneo ya gati, uboreshaji wa maeneo ya kuhifadhia mizigo pamoja na miundombinu ya barabara za ndani ya Bandari, jambo linalorahisisha upitishaji wa magari na mizigo.
Aidha, imeelezwa kuwa kuna ongezeko la matumizi ya Bandari ya Mtwara katika kuhudumia mizigo ya ndani na ya nchi jirani. Hali hii inaonesha kuimarika kwa uwezo wa Bandari katika ushindani wa kimasoko ambapo imeongeza mchango wake katika kukuza biashara na uchumi wa Ukanda wa Kusini mwa Tanzania pamoja na nchi jirani.
Vievile, imeelezwa kuwa juhudi zinaendelea kufanyika katika kuimarisha miundombinu ya TEHAMA ndani ya Bandari ili kuboresha usimamizi wa shughuli za kila siku. Mifumo bora ya kidijitali inasaidia kuongeza uwazi, kupunguza muda wa kuhudumia wateja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Hata hivyo, imebainishwa kuwa kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati ya Bandari ya Mtwara na wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi na biashara. Ushirikiano huu unasaidia kubaini changamoto kwa haraka na kuzifanyia kazi ikiwemo kuweka mikakati ya kuboresha huduma na miundombinu ya Bandari.
Kwa ujumla, kikao kimebainisha kuwa maboresho yanayoendelea katika miundombinu na usimamizi wa Bandari ya Mtwara yanaendelea kuongeza ufanisi wa huduma, kuvutia wateja zaidi na kuimarisha nafasi ya Bandari kama lango kuu na muhimu la biashara katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania na nchi jirani.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"