Sélectionnez votre langue

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a, ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa ufanisi mkubwa unaoendelea kuonyeshwa katika kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena zinazopitia bandari mbalimbali nchini.
Dkt. Chang’a ametoa pongezi hizo tarehe 3 Agosti, 2026, alipotembelea banda la TPA katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, kunakofanyika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) ambayo yalifunguliwa rasmi tarehe 1 Agosti, 2026, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba.
Amesema mafanikio yanayopatikana katika sekta ya bandari yana mchango mkubwa katika kukuza biashara, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuimarisha uchumi wa Taifa, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali za Serikali. Aidha, Dkt. Chang’a amepongeza ushirikiano uliopo kati ya TPA na TMA, hususan katika masuala ya hali ya hewa ambayo yana mchango mkubwa katika shughuli za kila siku za kibandari, ikiwemo usalama wa meli, upakiaji na upakuaji wa mizigo pamoja na utoaji wa taarifa muhimu kwa wadau wa sekta ya usafirishaji na biashara.
Kwa upande wake, TPA imeendelea kutumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali kuhusu huduma zinazotolewa katika bandari za Tanzania, maboresho ya miundombinu pamoja na fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana kupitia bandari.
Banda la TPA limeendelea kuwa kivutio katika Maonesho ya Nanenane kwa kupokea wageni wengi kutoka taasisi mbalimbali, sekta binafsi na wananchi wanaotembelea kwa lengo la kupata taarifa na ufafanuzi kuhusu huduma za bandari na mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.