Sélectionnez votre langue

Serikali imeshauriwa kuongeza maeneo zaidi yanayozunguka Mradi wa Usanifu na Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa/Mgao Mkoani Mtwara ili kuweka nafasi ya upanuzi wa Bandari hiyo siku zijazo na kuepusha gharama kubwa za fidia na ununuzi wa ardhi zitakazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya baadaye. Ushauri huo umetolewa tarehe 9 Septemba, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso (Mb) wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Bandari ya Kisiwa/Mgao. Mhe. Kakoso amesema uzoefu unaonesha kuwa kuchukua maeneo madogo wakati wa 
kuanzisha miradi mikubwa huweza kuongeza gharama pale inapohitajika kupanua miradi hiyo baadaye, hivyo Serikali inapaswa kuwa na mtazamo wa muda mrefu kwa kuhakikisha maeneo muhimu yanayozunguka mradi yanahifadhiwa mapema. Aidha, Kamati hiyo imesisitiza umuhimu wa kuanza kwa wakati ujenzi wa barabara ya kiunganishi cha lami itakayounganisha Bandari ya Kisiwa/Mgao na Mtwara ili kuhakikisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji inaenda sambamba na maendeleo ya Bandari na kuwezesha shughuli za Bandari kuanza mara tu baada ya kukamilika kwa mradi. Katika ziara hiyo, Kamati pia imeitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuendelea kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa kupanda mikoko katika maeneo yanayohusisha shughuli za ujenzi huku ikiitaka Serikali ya Mkoa wa Mtwara kuendelea kusimamia haki za msingi za wananchi, ikiwemo usalama kazini, usawa wa afya na matumizi sahihi ya fedha za Ushuru wa Huduma na Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Serikali itatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya Sekta ya Uchukuzi inayotekelezwa Mkoani Mtwara ili ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyokusudiwa. Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Dkt. Baraka Mdima, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA amesema Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa/Mgao unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 435 na unalenga kuongeza uwezo wa Bandari ya Mtwara kuhudumia mizigo mikubwa ikiwemo kupitia upanuzi wa miundombinu ya Bandari 
na kuongeza uwezo wa kuhudumia meli kubwa. Amesema mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 48 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2028 hatua inayotarajiwa kuimarisha nafasi ya Bandari ya Mtwara katika 
kuhudumia biashara na usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya Tanzania.