Sélectionnez votre langue

Kampuni ya saruji ya Dangote imetoa pongezi na kueleza kuridhishwa na maendeleo makubwa ya Bandari ya Mtwara pamoja na kiwango cha huduma kinachotolewa, huku ikiahidi kuongeza kiwango cha shehena ya saruji kitakachosafirishwa kupitia bandari hiyo kwenda katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Pongezi hizo zimetolewa na Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Bw. Adeyemi Fajobi, wakati wa ziara ya ujumbe kutoka Makao Makuu ya kampuni hiyo katika Bandari ya Mtwara tarehe 24 Juni, 2026. Ziara hiyo ililenga kujionea utekelezaji wa shughuli mbalimbali bandarini hapo pamoja na kufanya mazungumzo ya kibiashara yanayolenga kuimarisha usafirishaji wa saruji inayozalishwa na Kiwanda cha Dangote kupitia Bandari ya Mtwara.

Akiwakaribisha wageni hao, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand Nyathi, alisema bandari imeendelea kufanya maboresho makubwa ya miundombinu, vifaa na huduma, hatua iliyoongeza ufanisi wa kuhudumia shehena kwa haraka, usalama na ubora. Ahadi ya Kampuni ya Dangote kuongeza matumizi ya Bandari ya Mtwara ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa ushirikiano kati ya sekta ya bandari na viwanda. Ongezeko la usafirishaji wa saruji kupitia bandari hiyo linatarajiwa kuongeza biashara ya ndani na kimataifa, kuimarisha shughuli za uchumi wa bluu na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.