MAAFISA WA BANDARI YA MTWARA WAFANYA ZIARA YA KIKAZI ZPC
Maafisa wa Bandari ya Mtwara wakiongozwa na Meneja wa Bandari Bw. Ferdinand S. Nyathi wamefanya ziara ya kikazi Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) ambapo walipokelewa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu Bw. Khamis Salum Abdi.
Lengo kuu la ziara hiyo lilikuwa ni kutembelea wateja na wadau wa Bandari ya Mtwara waliopo Visiwani Zanzibar ili kukuza mahusiano yaliyopo, kukusanya maoni na mapendekezo pamoja na kujadiliana kuhusu changamoto zilizopo hususan wakati wa utolewaji wa huduma katika Bandari ya Mtwara.
Katika ziara hiyo, maafisa hao walipata fursa ya kutembelea wadau mbalimbali ikiwemo mwekezaji katika Bandari ya Zanzibar (ZMT) ambaye ni msimamizi mkubwa wa shughuli za uendeshaji wa Bandari hiyo.
Vilevile, walitembelea TP Company ambao ni miongoni mwa wateja wakubwa wa saruji ya Dangote inayosafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara na pia walitembelea Bandari ya Fumba.
Ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa wadau hao waliweza kueleza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika shughuli zao za kila siku. Maoni na mapendekezo yao yalipokelewa kwa ajili ya kufanyiwa kazi na uboreshwaji huduma. Aidha, maafisa wa Bandari ya Mtwara walipata fursa ya kujifunza mbinu tofauti za kuhudumia shehena, jambo ambalo litasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Kwa ujumla, ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha ushirikiano uliopo, kuwa chachu ya maboresho mbalimbali na mabadiliko chanya ya kibiashara katika Bandari ya Mtwara.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"