Sélectionnez votre langue

Na Mwandishi Wetu

Mpango wa uboreshaji miundombinu katika Bandari ya Mtwara unaotekelezwa kupitia Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, umeongeza ufanisi ambapo zaidi ya tani 100,000 za korosho zimesafirishwa katika msimu huu wa zao hilo.

Mafanikio hayo yamepatikana baada ya kuongezwa vifaa vya kupakia na kushusha mizigo, hivyo kuchangia ongezeko la idadi ya meli zinazotia nanga kwenye bandari hiyo hali inayotajwa kuchochea zaidi uchumi katika ukanda wa kusini.

Akizungumza mkoani Mtwara wakati wa ziara ya kukagua maboresho katika bandari hiyo, Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, alisema serikali inatekeleza mkakati huo wenye lengo la kukuza uchumi na kufungua fursa za ajira kwa wananchi.

"Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuweka msukumo kwenye usimamizi na ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya uchukuzi na ndiyo sababu meli zimeanza kuja kwa wingi," alieleza.

Profesa Mbarawa alibainisha kuwa kabla ya maboresho hayo bandari hiyo ilikuwa kwa siku ikipokea wastani wa meli moja, lakini sasa meli nyingi zaidi zimekuwa zikitia nanga.

"Leo kuna meli zipo zinapakia mizigo, moja ni ya tani 9,000 na nyingine ni tani 30,000. Kesho zitakuja meli zingine tatu zitakazofanyakazi kwa wakati mmoja. Vitendea kazi vimeongezeka zaidi na vingine vitaletwa hapa kutoka Bandari ya Dar es Salaam ambako mwekezaji ameleta mitambo mingine," alisisitiza.