Sélectionnez votre langue

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limeridhishwa na kuipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bandari Kavu ya Kurasini.

Mapema leo tarehe 4 Februari, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC

Bw. Mohamed Salum ametembelea mradi huo mkubwa unaotekelezwa na TPA na kuelezea kuridhishwa kwake na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji huku akihimiza mradi huo kukamilika kwa wakati ili kuboresha ufanisi wa bandari kwa kuongeza kasi ya huduma.

“Sisi TASAC tumekuja mapema kutoa maoni ya namna ya kuboresha ujenzi wa bandari hii na pia kujipanga kwa ajili ya kufanya ukaguzi. Mradi huu ukikamilika unaweza kuhudumia zaidi ya makasha 700,000, jambo ambalo ni faida kubwa kiuchumi na kutaleta mageuzi makubwa katika uwezo wa bandari yetu, hongera sana TPA.

Mradi huu unalenga kuongeza ufanisi wa kuhudumia makasha katika Bandari ya Dar es Salaam, ambayo kwa sasa inapokea shehena kubwa kutokana na maboresho ya miundombinu na mchango wa sekta binafsi katika kuhudumia meli.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed G. Abed ameishukuru TASAC kwa kutembelea mradi huo, na kubainisha kwamba eneo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 220,000 lipo katika hatua za mwisho za ukamilikaji.

“Bandari ya Dar es Salaam imefanya vizuri nusu ya Mwaka huu wa Fedha kuhudumia zaidi ya tani milioni 16 za shehena, tunatarajia Mradi huu utakapokamilika Aprili 2026 tutaongeza uwezo wa kupokea makasha mara mbili ya sasa, tutaongeza kasi ya meli kupakia na kuondoka, na kuvutia meli nyingi zaidi kutia nanga bandarini”, amesema Bw. Abed.

Mradi huu utakapokamilika utakuwa umeunganishwa moja kwa moja na barabara, na reli za SGR na MGR, sambamba na uwepo wa taasisi mbalimbali za serikali zinazotoa huduma bandarini ili kuharakisha utoaji huduma.

Ujenzi wa mradi huu unafanyika kwa Awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza inatarajiwa kukamilika Aprili 2026 ambapo huduma zitaanza kutolewa mara.