MKUU WA MKOA WA TANGA AFANYA ZIARA YA KUKAGUA UTENDAJI KAZI WA BANDARI YA TANGA

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, ameipongeza Bandari ya Tanga kwa utendaji wenye ufanisi mkubwa katika uhudumiaji wa meli na mizigo ya wateja.
Mhe. Balozi Burian, ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji wa Bandari ya Tanga.
Katika ziara hiyo Mhe. Balozi Burian alishuhudia meli mbili za mizigo mchanganyiko za MV. Eastern Edelweiss na MV. Zhong Chang Yun 6 zikiwa zinahudumiwa kwa ufanisi mkubwa.
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Salehe Mbega alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba, Bandari ya Tanga itaendelea kutoa huduma bora ili kuwavutia wateja wengi zaidi kutumia bandari hiyo.
Aidha pamoja na mafanikio hayo, Bw. Mbega alimuomba Mkuu wa Mkoa asaidie bandari ipate maeneo ya karibu na bandari ili kuiwezesha bandari hiyo kuhudumia shehena kubwa za mizigo mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa alimuhakikishia Meneja wa Bandari kuyapata maeneo hayo ili bandari iweze kuwa kitovu cha shughuli za kiuchumi kwa Mkoa wa Tanga, Taifa pamoja na nchi jirani.
Kwa upande wafanyakazi wa kutwa waliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika Bandari ya Tanga ambao umewezesha watu kupata fursa za ajira nyingi kutokana na kuongezeka kwa meli na shehena.