Sélectionnez votre langue

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mha. Dkt. Baraka R. Mdima, amewataka watumishi wapya wa TPA kutokuwa vikwazo katika utoaji wa huduma, bali wawe wawezeshaji wa wananchi na wadau mbalimbali kufanya biashara kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa, Kikanda na wa watu binafsi.

Mha. Dkt. Mdima ametoa wito huo tarehe 5 Februari 2026, alipokuwa akifunga rasmi mafunzo ya awali (Induction Course) ya siku nne kwa watumishi wapya wa TPA, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la TPA (OSC), jijini Dar es Salaam.

Amesisitiza kuwa TPA ni taasisi inayohudumia wateja wa kitaifa, kikanda na kimataifa, hivyo ni muhimu kwa watumishi wapya kutumia mafunzo waliyopewa kama dira ya kutoa huduma bora, kwa weledi na kwa kuzingatia maslahi mapana ya wateja na uchumi wa nchi kwa ujumla.

“Maamuzi, jitihada na juhudi mtakazoonesha katika utendaji wenu zijenge taswira chanya ya TPA ndani na nje ya Tanzania. Tusiwe vikwazo bali tuwe wawezeshaji wa watu kufanya biashara zao kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa Taifa, Kikanda na watu binafsi,” alisema Mha. Dkt. Mdima.

Aidha, amewasihi watumishi hao wapya kwenda kuwa mabalozi wema wa TPA kwa kutekeleza majukumu yao kwa kushirikiana, kwa uadilifu na weledi, sambamba na kuzingatia malengo na mikakati ambayo TPA imejiwekea ili kuhakikisha taasisi hiyo inafanikiwa katika majukumu yake.

Pia amewahimiza kutobweteka, bali kujenga utamaduni wa kujiendeleza kimasomo, kuuliza maswali na kushirikiana na wafanyakazi wenzao ili kuboresha utoaji wa huduma. Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uelewa kuhusu historia ya TPA na bandari zake, majukumu ya kisheria, Dira na Dhima ya TPA pamoja na Sheria, Kanuni na Miongozo inayosimamia utendaji kazi wa taasisi hiyo.