Sélectionnez votre langue

Tanga, Machi 1, 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuongeza ufanisi katika sekta ya bandari, ambayo ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Mhe. Rais Dkt. Samia ametoa wito huo leo alipofanya ziara katika Bandari ya Tanga kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa gati mbili mpya, unaolenga kuboresha uwezo wa bandari hiyo kushindana kimataifa.

“Bandari ni ushindani. Ni lazima mfanye kazi kwa bidii na kwa uadilifu mkubwa ili tuweze kuongeza ufanisi na kuvutia biashara zaidi,” alisema Mhe. Rais Dkt. Samia.

Ameeleza kuwa maboresho yanayoendelea katika bandari mbalimbali nchini yanahitaji watumishi wa TPA kuwa na ujuzi wa kisasa ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia, hivyo amewahimiza kujiendeleza kitaaluma ili kuongeza ufanisi na ushindani katika bandari.

Aidha, Mhe. Rais Dkt. Samia ameagiza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TPA kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na haki, akisisitiza kuwa hatavumilia vitendo vyovyote vinavyoweza kuhujumu uchumi kupitia bandari.

“Nimeridhishwa na hatua kubwa ya maboresho yanayoendelea katika bandari zetu, ikiwemo Bandari ya Tanga. Lazima tuhakikishe uwekezaji huu unawanufaisha Watanzania kwa kupunguza gharama za biashara na kuongeza ufanisi wa huduma,” aliongeza.

Akimkaribisha Mhe. Rais, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, alimpongeza kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha sekta ya bandari, akieleza kuwa uwekezaji unaoendelea umekuwa na matokeo chanya kwa uchumi wa nchi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa, alimweleza Mhe. Rais kuhusu hatua za utekelezaji wa mradi wa gati mbili mpya katika Bandari ya Tanga, akibainisha kuwa mradi huo utaongeza ufanisi wa upakuaji na upakiaji wa shehena.

Katika kutambua mchango wake wa kuimarisha sekta ya bandari, Bw. Mbossa alimkabidhi Mhe. Rais Tuzo ya Shukrani kwa uongozi wake thabiti na maelekezo yenye tija katika kuendeleza miundombinu ya bandari na kukuza uchumi wa Taifa.