Sélectionnez votre langue

Serikali imesema mpango wake ni kuhakikisha nchi zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam zinaunganishwa na reli ya kisasa ya SGR ili kurahisisha shughuli za Uchukuzi wa shehena kutoka bandarini.

 

Kauli hiyo imetolewa tarehe 25 Februari,2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof.Godius Kahyarara katika kikao kilichokutanisha ujumbe wa Gavana wa Jimbo la Manyema kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo( DRC) na Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) jijini Dar es Salaam.

 

Prof.Kahyarara amesema Serikali iko makini na mradi wa ujenzi wa reli hiyo na mpaka kufikia 2029 itakuwa imefika mkoa wa Kigoma.

 

Katika salamu zake Gavana wa Jimbo la Maniema Mhe.Moïse Mussa Kabwankubi aliyeambatana na wafanyabiashara kutoka nchini DRC,alisema shehena kubwa kutoka jimbo hilo inapitia katika Bandari za Tanzania na lengo la ujio wake ni kuangalia shughulia za uchukuzi wa shehena baina ya nchi hizi mbili.

 

Katika salamu zake Balozi wa Tanzania nchini DRC Mhe.Balozi Said Juma Mshana,alisema ni jambo la kujivunia kwamba Maraisi wa nchi zote mbili wameendelea kudumisha udugu baina ya nchi hizi unaochochea ukuaji wa biashara na sekta ya uchukuzi kwa ujumla.

 

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA,Mkurugenzi wa Mipango, Ubora na Vihatarishi Dkt. Boniphace Nobeji,alisema shehena ya DRC inayopita Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuongezeka na ndio maana ujenzi wa Bandari za kimkakati unafanyika ili kuhudumia mzigo wa nchi hiyo  kwa urahisi,zikiwemo Bandari za Kigoma,Karema na Dar es Salaam

.