Sélectionnez votre langue

Serikali imezitaka taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Uchukuzi kuangalia namna zinavyoweza kunufaika na uhusiano wa kibiashara katika sekta ya usafirishaji baina ya Tanzania na Misri.

 

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof.Godius Kahyarara katika kikao kilichokutanisha ujumbe wa Wataalamu wa Wizara ya Uchukuzi ya Jamhuri ya Kiarabu ya Misri na Uongozi wa Wizara ya Uchukuzi ya Tanzania kilichofanyika Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma lililopita. .

 

Prof. Kahyarara alitaja maeneo kadhaa yenye miradi ya bandari kama Bagamoyo,,Mwanza,Mbamba Bay,Kisiwa Mgao na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) itakayorahisisha Uchukuzi wa shehena kutoka bandarini.

 

Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi wa Misri Mhe. Mohamed Fathi alisema  ushirikiano baina ya Tanzania na Misri ni wa kihistoria na umekuwa ni ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi.

 

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA,Mkurugenzi wa Mipango,Ubora na Vihatarishi Dkt.Boniphace Nobeji alisema TPA  kupitia Serikali imekuwa ikishirikiana na Misri kwa muda mrefu kwenye eneo la mafunzo kwa watumishi na matarajio ni kuona ushirikiano ukiimarika kwenye eneo la shughuli za kibandari kwa ujumla.

 

Mara baada ya kikao hicho ,ujumbe huo ulipata fursa ya kufanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam ambako walilakiwa na Mkurugenzi wa Bandari hiyo Bw.Gallus Abed Gallus.