Sélectionnez votre langue

Na Mwandishi Wetu

Ushirikiano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Bandari ya Antwerp ya nchini Ubelgiji umepangwa kuimarishwa zaidi ili kuongeza tija na kufungua fursa zaidi za uwekezaji Bandarini.

Hayo yamebainika hivi karibuni mara baada ya ujumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Ubelgiji na Wawekezaji wa Bandari ya Antwerp kufanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ziara ya ujumbe, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa amesema ziara ya ujumbe huo umelenga kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya TPA na Bandari ya Antwerp.

Bw. Mbossa pia ametumia fursa hiyo kuelezea fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika Bandari zinazosimamiwa na kuongozwa na Mamlaka.

Maeneo mengine yatakayoguswa na ushirikiano huo, ni pamoja na maboresho ya huduma za Kibandari kulingana na Mkataba wa ushirikiano wa Bandari hiyo ya Antwerp na TPA.

Ushirikiano huo pia umelenga kujikita katika kutoa ushauri elekezi wa namna bora zaidi ya kuyafikia mabadiliko chanya ya huduma za Kibandari hapa nchini, pamoja na ushirikiano wa karibu na Jumuiya hiyo.

Aidha mazungumzo yao yamegusia nia njema ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Maboresho ya Bandari Nchini ambapo Bw. Mbossa ameulezea Ujumbe huo kuhusu fursa zilizopo za Uwekezaji katika Bandari za TPA.

Ujumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Ubelgiji, Wawekezaji na Wafanyakazi wa Bandari ya Antwerp uliofanya ziara bandarini, uliongozwa na Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Mhe. Peter Huyghebaert na Balozi wa Tanzania katika Ufalme wa Ubelgiji na Jumuiya ya Ulaya, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga ulifanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam kwaajili ya kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji katika Bandari hiyo.