Sélectionnez votre langue

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na waendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL), wameendesha kampeni ya kimasoko katika mji wa Lubumbashi, DR Congo.

Ziara hiyo ililenga kusikiliza changamoto za wateja na wadau wa biashara, pamoja na kuwasilisha maboresho makubwa yaliyofanywa katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Kigoma.

Akifungua mkutano huo, Konseli Mkuu wa Tanzania mjini Lubumbashi, Bw. Magubilo Muroba, alipongeza ushirikiano kati ya bandari za Tanzania na wafanyabiashara wa DR Congo, uliosababisha ongezeko la mizigo kwa asilimia 43 kutoka tani milioni 4.1 mwaka 2023/24 hadi milioni 5.9 mwaka 2024/25.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Josephat Lukindo, alisisitiza dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kutoa huduma za kisasa. Ushirikiano wa TPA na waendeshaji wake, ukiungwa mkono na uwekezaji wa mitambo ya kisasa, umefanya muda wa kuhudumia meli za makasha kupungua hadi wastani wa siku tatu.

Mbali na mkutano, ujumbe huo ulitembelea kampuni kubwa za usafirishaji ikiwemo Impala Cargo Terminal na Conexas Terminal, ambazo zote ziliridhishwa na huduma zitolewazo na kuahidi kuendeleza ushirikiano na bandari za Tanzania.

Uchaguzi 2025 Logo