Sélectionnez votre langue

Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekutana na ujumbe kutoka kampuni ya uwakala wa meli ya Inchcape Shipping Services katika kikao kilicholenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa kibiashara na kuboresha huduma za usafirishaji na uhudumiaji wa shehena kupitia Bandari ya Mtwara. Kikao hicho kilifanyika Septemba 3, 2026, Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam, na kuongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mha. Dkt. Baraka Mdima, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA. Katika kikao hicho, pande hizo mbili zilijadili fursa mbalimbali za kuendeleza ushirikiano, hususan katika kuongeza ufanisi wa huduma za bandari, kuvutia na kuongeza shehena kupitia Bandari ya Mtwara, pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wadau wa sekta ya usafirishaji.

ha. Dkt. Mdima alisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na kampuni za uwakala wa meli na wadau wengine wa sekta ya usafirishaji, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kukuza biashara, kuongeza ushindani na kuimarisha nafasi ya Bandari ya Mtwara katika kuhudumia biashara ya ndani na ya kikanda. Kwa upande wake, ujumbe wa Inchcape Shipping Services ulieleza dhamira ya kampuni hiyo ya kuendelea kushirikiana na TPA katika kuboresha huduma na kutafuta fursa mpya za kuongeza ufanisi pamoja na matumizi ya Bandari ya Mtwara. TPA inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha miundombinu na huduma katika bandari zake, ikiwa ni pamoja na Bandari ya Mtwara, kwa lengo la kuongeza ufanisi, kuvutia shehena zaidi na kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi nchini.