Sélectionnez votre langue

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imezihakikishia Nchi zinazohudumiwa na Bandari za Tanzania chini ya TPA kuwa, itaendelea kuunga mkono juhudi na jitihada za kuimarisha biashara ya kikanda na kukuza uchumi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA katika ufunguzi wa Mkutano wa tano wa Juma la Shughuli za Kibandari na Forodha “Ports & Customs Week 2024“uliofanyika tarehe 3 hadi 4 Desemba,2024 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano Dkt. George Fasha, amesema nia hiyo ya TPA inaenda sambamba na ukuaji wa maendeleo ya teknolojia pamoja na matokeo chanya kwa Bandari na mifumo ya forodha na kuimarisha ushirikiano ili kuendeleza na kuwezesha biashara na kukuza uchumi miongoni mwa nchi zinazotumia Bandari za Tanzania.

Mkutano huu wa Shughuli za Kibandari na Forodha ni muhimu kwani unatoa suluhu za kiteknolojia kwa changamoto zinazokabili bandari na mamlaka ya forodha barani Afrika ukiwa unaongozwa na kaulimbiu ya “Kuimarisha Ushirikiano wa Kikanda na Uwekaji mifumo ya Kidijiti wa Mipaka, Bandari na Forodha.