Sélectionnez votre langue

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dk.Toba Alnason Nguvila, ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa ushiriki wake katika Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma 2026, akieleza kuwa ushiriki huo unaonesha dhamira ya Mamlaka hiyo katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa Umma. Dk.Toba ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la TPA katika kongamano hilo linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), lililoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Amesema TPA imeendelea kuwa mfano wa Taasisi inayozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Ununuzi wa Umma, hatua inayochangia upatikanaji wa thamani halisi ya fedha za Umma, kuimarisha uwazi na kudumisha uadilifu katika matumizi ya rasilimali za Serikali. Kongamano hilo linaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Kutumia Fursa ya Ununuzi wa Umma Kidijitali Kufikia Uchumi Endelevu, Jumuishi na Shindani Kuelekea Dira ya Tanzania 2050.”
Kupitia ushiriki wake katika kongamano hilo, TPA inaendelea kuonesha dhamira ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha mifumo ya ununuzi wa Umma na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa kupitia utoaji wa huduma za Bandari zenye ufanisi na zinazozingatia misingi ya utawala bora.