Sélectionnez votre langue

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 30 Aprili 2025, amefungua rasmi Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Mawakala wa Forodha Afrika Mashariki na Kati unaofanyika Kisiwani Unguja, Zanzibar na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa katika sekta ya forodha ili kuchochea maendeleo ya biashara na uchumi wa dunia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wadau kutoka mataifa mbalimbali, Mhe Abdulla amesema Serikali ya Tanzania  Bara na Visiwani  zimejipanga kuboresha zaidi mazingira ya biashara kwa kuimarisha mifumo ya forodha, Miundombinu ya Uchukuzi katika nyanja zote ,kupunguza vikwazo vya  kikodi na visivyo vya kikodi sambamba na matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kuhakikisha huduma bora na za haraka kwa mustabali mpana wa Uchumi wa Tanzania na nchi jirani zinazotumia bandari za Tanzania.

Katika kusisitiza dhamira njema ya Serikali, amesema, Tanzania Bara na Zanzibar, zimewekeza katika miundombinu ya kisasa kama vile bandari, reli na barabara ili kuhakikisha ufanisi wa huduma za forodha na usafirishaji wa shehena.

Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, amesema Tanzania inaendelea kuimarisha miundombinu ya uchukuzi ili kuifanya nchi kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt Khalid Salum Mohammed, amebainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza mikakati ya kuimarisha bandari na mifumo ya forodha visiwani humo kwa lengo la kuifanya Zanzibar kuwa lango muhimu la biashara za kimataifa.

Awali Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mawakala wa Ushuru na Forodha (FIATA) Bw. Turgut Erkeskin amesifu juhudi zinazofanywa na Tanzania Bara na Zanzibar katika kuboresha sekta ya forodha.