Sélectionnez votre langue

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya kikanda kwa kushiriki kikamilifu katika mkutano wa Land-Linked Zambia 2026, mjini Lusaka, nchini Zambia.

Ushiriki wa TPA, unalenga moja kwa moja kuongeza shehena ya mizigo inayopitia katika Bandari ya Dar es Salaam, ambayo ni lango kuu la biashara kwa nchi zisizo na Bandari kama Zambia.

Mkutano huo unaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji na biashara, wakiwemo Serikali, Mamlaka za Bandari, Waendeshaji wa Reli, na Wawekezaji wa miundombinu.

Kupitia jukwaa hilo, TPA inapata fursa ya kuonesha maboresho yaliyofanyika katika Bandari zake, ikiwa ni pamoja na kuongeza kina cha maji, kupanua magati, na kuboresha mifumo ya kidijitali ya kuhudumia mizigo kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.

Kwa Zambia, ambayo uchumi wake unategemea kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa madini kama shaba, upatikanaji wa njia ya uhakika na yenye gharama nafuu kwenda baharini ni jambo la msingi.

Hapa ndipo umuhimu wa TAZARA Railway unapojitokeza, ukiunganisha moja kwa moja maeneo ya uzalishaji nchini Zambia na Bandari ya Dar es Salaam. Ushiriki wa TPA katika mkutano huu pia unalenga kuimarisha matumizi ya reli hiyo ili kuongeza ushindani wa ukanda huu wa usafirishaji.

Aidha, mkutano wa Land-Linked Zambia unatoa fursa kwa TPA kujitangaza katika mazingira ya ushindani mkali kutoka bandari nyingine za kikanda kama zile za Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini na Angola (Lobito corridor).

Katika ushindani huu, ubora wa huduma, kasi ya upakuaji na upakiaji mizigo, pamoja na gharama za usafirishaji, ni vigezo muhimu vinavyoamua mwelekeo wa wafanyabiashara na wasafirishaji wa mizigo.

Kwa kushiriki katika mkutano huu, TPA inalenga kuvutia wateja zaidi kutoka Zambia na nchi jirani, kuongeza kiwango cha mizigo kinachopitia bandarini, na hivyo kuongeza mapato ya taifa.

Hatua hii pia ina mchango mkubwa katika kukuza ajira, kuimarisha uchumi wa nchi, na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Kwa ujumla, ushiriki wa TPA katika mkutano wa Land-Linked Zambia 2026 ni mkakati mahsusi wa kukuza biashara, kuimarisha ushirikiano wa kikanda, na kuongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam katika soko la kimataifa.

Lakini pia ni hatua inayoonesha wazi kuwa Tanzania ipo tayari kunufaika kikamilifu na fursa zinazotokana na dhana ya “land-linked,” kwa kuifanya Zambia na nchi nyingine zisizo na bandari kuwa washirika wakuu wa maendeleo ya uchumi wa taifa.