Sélectionnez votre langue

Serikali ya Jamhuri ya Zambia imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina yake na Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati wa Zambia Prof.Ephraim Munshifwa alipofanya ziara Bandari ya Dar es Salaam katika eneo linalohudumia meli za mafuta Kurasini Oil Jet (KOJ) na kwenye boya linaloelea baharini (Single Mooring Point - SPM) Januari 16,2026.

Katika salamu zake za ukaribisho alizozitoa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce M Mbossa, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed ameishukuru nchi ya Zambia kwa kuendelea kutumia Bandari ya Dar es Salaam na kuainisha kuwa ufanisi wa Bandari umeongezeka kutokana na uwekezaji uliofanyika kwenye miundombinu sambamba na ushirikishwaji wa waendeshaji binafsi katika Bandari.

Aidha, Bw. Gallus ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia tani milioni 27.7 na mwaka 2025/2026 inatarajia kuhudumia zaidi ya tani milioni 32. Ongezeko hili linatokana na ufanisi pamoja na imani ya wateja kwa huduma za Bandari ya Dar es Salaam.

Tanzania na Zambia zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu wa kibiashara kupitia mradi wa bomba la mafuta la Tanzania - Zambia (TAZAMA) lenye urefu wa kilometa 1710 linaloanzia Dar es Salaam mpaka Ndola Zambia.