Sélectionnez votre langue

Viongozi wa Serikali za Wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya jijini Dar es Salaam, Septemba 4 na 5, 2026, wametembelea Bandari ya Dar es Salaam na Bandari kavu ya Kwala, kwa lengo la kujifunza na kujionea kwa vitendo utekelezaji wa miradi hiyo na mchango wake katika kukuza biashara, uwekezaji na uchumi wa Taifa. Ziara hiyo imewapa viongozi hao fursa ya kutembelea na kupata maelezo kuhusu maendeleo ya Mradi wa Usanifu na Ujenzi wa Gati la Malindi katika Bandari ya Dar es Salaam, Mradi wa eneo la zamani la EPZA Kurasini, Mradi wa kuhifadhi na kusambaza mafuta wa Farm Tank uliopo Kigamboni pamoja na Bandari kavu ya Kwala iliyopo Kibaha Aidha, viongozi hao walitembelea Bandari Kavu ya Kwala, ambako walipata fursa ya kufahamu namna bandari kavu inavyounganisha shughuli za bandari na maeneo ya ndani ya nchi, kurahisisha usafirishaji na usambazaji wa mizigo, kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi wa mnyororo wa usafirishaji.

Miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya uchukuzi na kuweka mazingira bora zaidi kwa biashara na uwekezaji, huku ikilenga kuongeza uwezo wa kushughulikia mizigo, kuboresha huduma na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa. Katika ziara hiyo, viongozi hao walielezwa umuhimu wa miradi hiyo katika kuongeza ufanisi wa shughuli za bandari, kurahisisha usafirishaji na uhifadhi wa mizigo, pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya bandari, reli na vituo vya kuhudumia mizigo vilivyopo ndani ya nchi. Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mha. Erick Madinda, ambaye alikuwa mwenyeji wa viongozi hao kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, alisisitiza umuhimu wa vijana, hususan wanafunzi wa vyuo vikuu, kuwa na uelewa mpana kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini na namna inavyochangia katika uchumi wa Taifa.

Ziara hiyo pia imelenga kuwawezesha viongozi hao kupata taarifa sahihi na kuzifikisha kwa wanafunzi wenzao pamoja na jamii kwa ujumla, hususan kuhusu utekelezaji, umuhimu na manufaa ya miradi ya kimkakati katika sekta ya uchukuzi. Kwa upande wao, viongozi hao wamepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuendeleza miundombinu ya bandari, reli na maeneo ya kuhudumia mizigo, wakieleza kuwa ziara hiyo imewapa fursa muhimu ya kuongeza maarifa na kuona kwa vitendo namna miradi mikubwa ya kitaifa inavyotekelezwa. Wamesema wataendelea kutumia nafasi zao kama viongozi wa wanafunzi kuwaelimisha wenzao kuhusu fursa zinazotokana na maendeleo ya sekta ya uchukuzi, ikiwemo biashara, ajira, uwekezaji, teknolojia na ubunifu. Kwa ujumla, ziara hiyo imekuwa darasa la vitendo kwa viongozi hao, likiwaunganisha moja kwa moja na miradi inayobeba sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania kuanzia bandarini, vituo vya kuhifadhi na kusambaza mizigo hadi kwenye bandari kavu zinazounganisha Bandari ya Dar es Salaam na maeneo ya ndani ya nchi. 
TPA inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo vijana na taasisi za elimu, katika kuongeza uelewa kuhusu shughuli na miradi ya bandari na mchango wake katika kuchochea biashara, uwekezaji na maendeleo ya Taifa.