WADAU WAUNGA MKONO ADA YA UENDELEZAJI WA MIUNDOMBINU MIPYA YA BANDARI (PID)
Wadau wa sekta ya usafirishaji na biashara katika Bandari ya Mtwara, wameonyesha kuunga mkono utekelezaji wa Ada ya Uendelezaji wa Miundombinu mipya ya Bandari (PID), wakieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuboresha huduma za bandari na kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.Wakizingumza kwa nyakati tofauti Mkoani Mtwara, Juni 2,2026, Wadau hao wamesema maboresho ya miundombinu ya bandari yataongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo, kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya usafirishaji na biashara.Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetangaza kuwa ada hiyo itaanza kutumika rasmi kuanzia Julai 1, 2026, baada ya kufanyika kwa mashauriano ya kina na wadau mbalimbali wa sekta husika.
Akizungumza Mkoani Mtwara, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand Nyathi, amesema TPA imepokea maoni ya wadau na kufanya marekebisho ya kiwango cha ada hiyo kutoka asilimia 9 iliyopendekezwa awali hadi asilimia 4.5 ya kodi ya forodha, hatua iliyolenga kupunguza athari na gharama kwa wafanyabiashara huku ikihakikisha upatikanaji wa fedha za maendeleo ya miundombinu mipya ya bandari. Bw. Nyathi amebainisha kuwa mapato yatakayokusanywa kupitia tozo hiyo yataelekezwa katika kuboresha miundombinu ya bandari, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kuimarisha ushindani wa bandari za Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.TPA imewahimiza wadau wote kuendelea kujipanga kwa utekelezaji wa tozo hiyo, ikisisitiza kuwa lengo kuu ni kuimarisha uwezo wa bandari za Tanzania kuhudumia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya uchumi unaokua kwa kasi.

EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"