Sélectionnez votre langue

Wafanyakazi wa Bandari ya Mtwara wamepatiwa semina ya mafunzo kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, magonjwa ya kuambukiza na afya ya akili. Semina hiyo ilifunguliwa rasmi na Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara Bw. Shaibu Salum Mdoe ambapo imefanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 29 na 30 Juni, 2026 katika Ukumbi wa Klabu ya Bandari Mtwara. Semina hiyo imeendeshwa na Madaktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Ligula wakiongozwa na Dkt. Renatus Morris Makarious kwa kushirikiana na Daktari wa Bandari ya Mtwara Dkt. Betrida Ntunaguzi.Katika semina hiyo, Madaktari hao waliwasisitiza wafanyakazi kuzingatia mfumo mzuri wa maisha kwa kula lishe bora, kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, kupunguza matumizi ya vilevi pamoja na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara. Aidha, walieleza kuwa hatua hizo zitasaidia kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali na kuongeza muda wa kuishi (Life span) katika afya njema hali itakayowawezesha kuendelea kuwa na afya bora na kuongeza tija kazini. Semina hiyo imefungwa rasmi na Kaimu Meneja wa Bandari ambapo katika hotuba yake amewakumbusha wafanyakazi kuwa afya ni mtaji muhimu wa maisha yao na maendeleo ya taasisi. Alisisitiza kuwa bila afya njema haiwezekani kufanya kazi kwa ufanisi wala kujenga maisha bora kwa familia na jamii. Aidha, aliwahimiza washiriki kuyafanyia kazi maarifa waliyoyapata ili mafunzo hayo yawe chachu ya mabadiliko chanya katika maisha yao binafsi na sehemu zao za kazi.