Sélectionnez votre langue

Katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani  kwa mwaka 2026 Watumishi Wanawake wa Bandari ya Tanga waliungana na Wafanyakazi  Wanawake wa kutwa wa bandari hiyo kufanya matendo ya huruma.

 

Wanawake hao, walitoa msaada wa Mashine za  kusaidia upumuaji  aina ya “C- PAP  Bubble Neonates, Oxygen Flowmeter” pamoja   na vifaa mbalimbali  katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo vyenye thamani ya Shilingi Milioni 5.

 

Akizungumza wakati wa kukabidhi Mashine hizo, Afisa  Mkuu Rasilimali Watu wa Bandari hiyo, Bi. Sharifa Nuhu  alisema, wamekuwa na utaratibu wa kila mwaka kutumia siku hiyo kufanya matendo ya huruma kwa jamii  na mwaka huu wasaidie Hospital ya Rufaa ya Mkoa, Bombo.

 

“ Mwaka huu tumeona tuunge mkono juhudi za Serikali katika kuboresha afya za watoto, hivyo tukaona tutoe msaada wa Mashine hizo katika wodi ya watoto wachanga katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo sababu ndio hospitali  kubwa ambayo hata wagonjwa  kutoka hospitali za Wilaya hupewa rufaa ya kuja hapa kufanya uchunguzi zaidi wa kitabibu”. Aliongeza Bi. Nuhu.

 

Awali akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa, Dkt . Abdi Msangi  aliwashukuru Watumishi hao kwa msaada walioutoa kwani umetolewa wakati muafaka kutokana na uwepo wa upungufu wa mashine hizo  katika wodi ya watoto wachanga wenye matatizo ya upumuaji.

 

Aidha Daktari Bingwa wa  Watoto katika Hospitali hiyo, Dkt. Mohamed Salehe alisema kuwa  Mashine hizo  zitakuwa msaada mkubwa hospitalini hapo ikizingatiwa kwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wanaozaliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na shida ya upumuaji. Kwa hiyo vifaa hivyo vitaenda kuboresha huduma ya upatikanaji wa huduma katika wodi ya watoto.

 Awali wanawake hao waliungana na wanawake wa Mkoa wa Tanga katika maandamano ya kuadhimisha  Siku ya  Wanawake  Dunia Kiwilaya yaliyofanyika katika uwanja wa Sekondari ya Usagara ambapo kauli mbiu ya mwaka 2026 inasema “ Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana, Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050