Sélectionnez votre langue

Serikali imetoa wito kwa wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wote wa sekta ya usafirishaji kushiriki katika hafla ya uzinduzi wa Bandari kavu ya Kwala iliyopo Vigwaza Mkoa wa Pwani, unaotarajiwa kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 31,2025. 

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Julai 25,2025, Makao makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, amesema hafla ya uzinduzi wa Bandari kavu ya Kwala ni ya kitaifa na itaenda sambamba na uzinduzi wa usafirishaji wa Shehena kwa treni ya SGR Kati ya Dar es Salaam na Dodoma pamoja na upokeaji wa mabehewa ya mizigo ya Treni ya Kawaida (MGR) ambapo mabehewa 50 ni mapya na mabehewa 20 yaliyokarabatiwa kwa ufadhili wa Wakala wa Uwezeshaji wa Ushoroba wa Kati (CCTTFA). 

“Rais wetu mpendwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, atazindua rasmi bandari hii muhimu kwa taifa letu, pamoja na huduma za kisasa za usafirishaji wa mizigo. Huu ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha uchumi wa viwanda kupitia miundombinu madhubuti ya uchukuzi,” amesema Mhe. Waziri Prof. Mbarawa.

Mhe. Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa bandari hiyo imejengwa kwa lengo mahsusi la kuongeza ufanisi katika kushughulikia shehena zinazowasili katika Bandari ya Dar es Salaam hasa baada ya maboresho makubwa yaliyofanyika kwenye bandari hiyo. 

“Kupitia Bandari Kavu ya Kwala, tunategemea ufanisi mkubwa katika kuhudumia shehena. Hii itasaidia kuongeza mapato ya Serikali kutokana na huduma zitolewazo katika Bandari ya Dar es Salaam na Kwala, huku tukipunguza gharama za uendeshaji kwa wafanyabiashara na kuwa kivutio kikubwa kwao kutumia Bandari ya Dar,” amesema Waziri Mbarawa.

Mhe. Waziri ameongeza kuwa hatua hii pia itaongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, hasa ikizingatiwa kwamba nchi jirani nazo zinawekeza kwa kasi katika bandari zao.

Faida nyingine zilizotajwa na Mhe. Waziri ni pamoja na kupungua kwa msongamano wa magari barabarani hususan Barabara ya Mandela na maeneo ya karibu na Bandari ya Dar es Salaam, kuimarika kwa usalama barabarani na kupungua kwa gharama za matengenezo ya barabara zinazoharibiwa na malori ya mizigo.

Aidha Mhe. Waziri amesisitiza kuwa ujio wa Bandari Kavu ya Kwala umeanza kuleta matumaini kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani, ambapo tayari kunashuhudiwa ongezeko la shughuli za kiuchumi, ajira kwa wananchi wa eneo hilo na matarajio ya uwekezaji wa viwanda kutokana na uwepo wa miundombinu madhubuti ya usafirishaji kuelekea Bandari ya Dar es Salaam.

Waziri Prof. Mbarawa pia amewahimiza 
wadau hao kuchangamkia fursa zitakazopatikana kupitia huduma za gharama nafuu na ufanisi wa muda mfupi zinazotolewa na Bandari Kavu ya Kwala, treni za kisasa za SGR na mabehewa mapya ya MGR.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) Bw. Plasduce Mbossa, amesema ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam, huku ikiendelea kuboresha na kupanua miundombinu ya bandari nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi na ushindani wa kitaifa na kikanda.

“ Bandari Kavu ya Kwala ni jitihada na mkakati madhubuti wa kitaifa unaolenga kuondoa changamoto sugu ya msongamano wa mizigo Bandarini na maeneo ya barabara ya Mandela Jijini Dar es Salaam.” amesema Bw. Mbossa.