Welcome to Tanzania Ports Authority
TICTS Kuilipa TPA Dola Milioni 14 Kodi ya Pango Kutoka Dola Milioni 7
Julai 06, 2017:
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni Binafsi inayoendesha Kitengo cha Kontena ndani ya Bandari ya Dar es Salaam, TICTS zimetia saini mkataba mpya wa ambapo TICTS watakuwa wakiilipa TPA kodi ya pango (rental fee) Dola Milioni Kumi na Nne (14) kwa mwaka kutoka Dola Milioni Saba (7) za awali.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (Mb.) ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo la utiaji saini amesema, “mbali na TICTS kulipa dola milioni 14, kodi hiyo pia itakuwa ikipanda kila mwaka kwa asilimia 3.8, hii inamaanisha kwamba kwa mwaka huu wakilipa dola milioni 14 mwakani watalipa dola milioni 14.8 na itaendelea kupanda kwa kiwango hicho kila mwaka.”
Prof. Mbarawa amesema tangu mwaka 2016 TICTS walikuwa wakilipa malipo ya aina mbili ambapo walikuwa wakilipa kodi ya pango Dola Milioni Saba (7) na kodi nyingine inayolipwa kwa kontena (throughput charges).
“Haijawahi kutokea leo unapangisha nyumba yako kwa shilingi laki moja kesho unamwambia mpangaji akulipe shilingi laki 2 akubali kwa urahisi, kwa hiyo TICTS sasa wamekubali kulipa dola milioni 14 kwa mwaka kutoka dola milioni saba, na zamani ilikuwa ukishaweka bei wanaendelea kulipa hiyohiyo lakini sasa kila mwaka itapanda kwa asilimia tatu (3),” ameongeza Prof. Mbarawa.
Kuhusu kodi ya kontena (kasha) TICTS sasa watakuwa wakilipa dola 20 kwa kila kontena na itakuwa ikiongezeka kwa asilimia nne (4) kila mwaka. Serikali imeiagiza pia TICTS kuhakikisha kwamba biashara ya bandari inakuwa na biashara ya kuhudumia kontena inakuwa kwa asilimia 6.5.
Mbali na ongezeko la mapato hayo pia eneo la ICD ya Ubungo ambalo lilikikuwa likitumiwa na TICTS sasa limerudishwa TPA na litakuwa mali ya Mamlaka. Mkataba baina ya TPA na TICTS ulisainiwa kwa mara ya kwanza mwaka 2000 kwa miaka 10 ambapo mwaka 2015 mkataba huo uliongezwa tena kwa miaka 15 na ulitakiwa kuisha mwaka 2025.
Kusainiwa kwa mkataba huu mpya ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Maguuli alilolitoa hivi karibuni wakati wa ziara yake bandarini. Katika ziara yake hiyo Mheshimiwa Rais aliiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuupitia upya mkataba wa TICTS na mnamo tarehe 6 mwezi 10, 2016 Waziri Mbarawa aliunda timu ambayo leo hii imekamilisha kazi hiyo kwa moyo wa kizalendo.