Na Mwandishi Wetu Serikali imeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kutekeleza kwa ufanisi mradi wa upanuzi na maboresho ya Bandari ya Tanga ambao umefikia asilimia 99.5. Akizungumza bandarini hapo wakati wa ziara yake kukagua mradi wa maboresho wa bandari hiyo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa amesema maboresho hayo yalikuwa na tija sababu bandari hiyo imekaa kimkakati zaidi. “Bandari hii imekaa kimkakati zaidi kutokana na kutoa huduma nchini na nchi jirani kama vile DR Congo na Burundi,” amesema. DR Congo ndio soko kubwa kwa bidhaa zinazopita katika Bandari za Tanzania. Mradi wa maboresho wa Bandari ya Tanga ambao mpaka sasa umefikia asilimia 99.85%, umelenga kuongeza uwezo wa bandari hiyo na kuboresha Zaidi ufanisi katika kuhudumia wateja. Mbali na kuipongeza TPA, pia amewataka wafanyakazi wa Bandari ya Tanga kuongeza juhudi katika kazi zao ili wateja wanaotumia Bandari hiyo waendelee kuamini kuwa Bandari ya Tanga ni yenye ufanisi na mahali salama kwa mizigo hao. Katika hatua nyingine Waziri Mkuu, ameendelea kusisitiza kuwa kama Serikali itaendelea kuzipa nafasi Sekta binafsi kutoa huduma katika bandari ili huduma za utoaji mizigo ziweze kuharakishwa ikiwemo meli kukaa muda mfupi bandarini. Mwisho