Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefurahishwa na ufanisi wa kiutendaji katika Bandari ya Mtwara hasa baada ya maboresho makubwa kufanyika katika Bandari hiyo. Akizungumza na Watumishi wa Bandari ya Mtwara baada ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Maboresho wa Bandari hiyo, Rais Dkt. Samia amesema Maboresho makubwa yaliyofanyika Bandarini hapo yameongeza ufanisi na kuufungua kiuchumi Mkoa wa Mtwara na Mikoa ya Kusini mwa Tanzania. “Serikali yangu itaendelea kuongeza Bajeti ya kuboresha miundombinu ya Bandari ili kuvutia zaidi wateja, wadau wafanyabiashara wa usafirishaji bidhaa mbalimbali ili kuongeza ushawishi wa kuzitumia zaidi Bandari zetu,” amesema Rais Dkt. Samia. Vilevile, Rais Dkt. Samia amesema Serikali yake imejiandaa kusafirisha Korosho kupitia Bandari ya Mtwara, hivyo ametoa wito kwa Wananchi kujiandaa kuiunga mkono Serikali kwa kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za Bandari. Rais Dkt. Samia pia ametoa rai kwa watumishi wa Bandari ya Mtwara kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili Bandari hiyo ifikie kiwango cha Bandari ya Dar es Salaam. Miradi iliyotekelezwa ni sehemu ya maboresho ya utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara ni pamoja na ujenzi wa Gati namba 2 lenye urefu wa mita 300, ujenzi wa mita ya kupakua na kupimia mafuta ili kuhakikisha mafuta yanayoshushwa katika Bandari ya Mtwara yana ubora stahiki Pamoja na ujenzi wa sehemu ya kuhifadhi makasha na ukarabati wa ghala na vifaa vya kuhudumia mizigo Bandarini. Mwisho