Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imetwaa tuzo ya kuwa mwajiri bora wa mwaka kwa mwaka 2023 kwa taasisi za umma hapa nchini. Akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Meneja Rasilimali Watu wa TPA, Bw. Said Msabimana amesema kwamba mafanikio hayo hayakuja hivi hivi bali yametokana na mifumo bora ya uajili waliojiwekea kama TPa, Huu ni mwaka wa pili mfululizo kwa TPA, kutwaa tuzo hizo zinazoandaliwa na kusimamiwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na kufanyika kila mwisho wa mwaka. Kwa mujibu wa wandaaji wa tuzo hizo, lengo la kuanzishwa kwake ni katika harakati za kutambua wanachama wanaofanya vizuri katika kuweka mikakati bora yenye kuthamini usimamizi wa rasimali watu na shughuli za biashara. Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka imeendelea kuwa tukio muhimu linalotambulika katika ngazi ya kitaifa ambapo kwa miaka kadhaa sasa tuzo hizi zimehamasisha Waajiri kuweka sera bora za ajira na usimamizi wa rasilimali watu. Mkurugenzi Mkuu wa Chama Cha Waajiri Tanzania, Bi. Suzanne Ndomba amesema wakati wa utoaji wa tuzo hizo kuwa zimeweza kuchochea na kuongeza tija, mahusiano bora mahala pa kazi, utii wa sheria na ushindani kibiashara. Awali akizungumza mchakato mzima ulivyokuwa, Bi Ndomba alisema makampuni shiriki yaliwasilisha madodoso mawili yaliyojazwa, moja likiwa limejazwa na Uongozi au Mkurugenzi Mkuu au Mkuu wa kitengo cha usimamizi wa Rasilimali Watu na dodoso jingine likiwa limejazwa na Mwajiriwa wa kawaida au Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi. Kwa mwaka huu, uzinduzi wa rasmi wa mchakato wa kutafuta Mwajiri Bora wa Mwaka kwa mwaka 2023 uliofanyika mwezi Mei 30,2023. Mwisho