Bandari ya Tanga na Bandari nyingine za Bahari za Kaskazini

Bandari ya Tanga ilijengwa mwaka 1914 awali ili kuhudumia mahitaji ya kibiashara na kilimo kaskazini mwa Tanzania. Bandari ya Tanga iko katika pwani ya kaskazini mwa Tanzania. Tanga ni moja ya bandari kongwe inayomilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ipo kaskazini mwa Tanzania. Bandari hii inasimamia pia bandari nyingine ndogo za Pangani, Kipumbwi, Kigombe na Mkwaja.

Bandari hii imeunganishwa vyema na barabara zinazotoka kaskazini na kati ya Tanzania na kuingia mkoani Tanga na hivyo kurahisisha usafiri kwenda mikoa hiyo na nchi jirani. Aidha bandari hii inaunganishwa upande wa kusini na bandari ya Dar es salaam kwa umbali wa kilomita 354.

Sifa za Bandari ya Tanga

Kila bandari ina sifa zake za kipekee ambazo zinachochea utendaji na ufanisi wa utoaji huduma bandarini. Zifuatazo ni baadhi ya sifa muhimu za Bandari ya Tanga.

  • Bandari hii ipo kimkakati zaidi kutokana na eneo ilipo. Yenyewe inahudumia mikoa ya kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Kanda ya Ziwa na nchi za jirani za Rwanda, Burundi na sehemu ya kusini ya Uganda
  • Ina kina kikubwa na mlango mpana wa kutosha kuingiza meli yenye kina chochote
  • Haina kipingamizi cha maji kupwa na kujaa kwa meli zinazoingia na kutoka bandarini
  • Ina ghuba ya asili inayokinga meli hivyo kuwezesha huduma kufanyika bila hofu.

Nyenzo za Bandari

Ukuta wa Gati

Bandari ya Tanga ina ukuta wa gati la kisasa wenye urefu wa mita 381 unahusu wa kwanza na wa pili. Ukuta wa kwanza ulikuwa na urefu wa mita 240 ulijengwa mwaka 1918 na sehemu iliyobaki mwaka 1954.

Miundombinu ya Bandari

Bandari ya Tanga ina mabanda matatu yaliyoezekwa kwa ajili ya shehena zinazoathiriwa na hali ya hewa.

  • Bandari ya Tanga ina gati mbili za kisasa zenye jumla ya urefu wa mita 450. Pia kuna mabomba mawili ya inchi 12 ambayo hutumika kupakua shehena za mafuta. Mfumo wa Conventional Buoy Mooring (CBM) umewekwa katika kisiwa cha Totten kwa ajili ya kuhudumia shehena ya gesi ya kupikia, (Liquefied Petroleum – LPG-). Mfumo huu umeungwa kwa njia ya mabomba yaliyounganishwa chini ya bahari hadi nchi kavu.
  • Kuna eneo la sakafu ngumu linalopokea shenena mchanganyiko la ukubwa wa meta za mraba 29,000
  • Yapo maghala matatu yenye jumla ya ukubwa wa meta za mraba 13,800
  • Kuna eneo maalumu la matengenezo ya vyombo vya baharini (chelezo)
  • Kuna eneo la kuhudumia meli za abiria.
 

Vifaa

Uhai wa bandari unategemea vifaa vilivyopo. Bila ya vifaa hakutakuwa na shughuli za bandari. Bandari ya Tanga ina vifaa lukuki vya kuhudumia shehena za aina mbalimbali:-

  • Winchi za bandarini (Habours Mobile cranes) sita zenye uwezo wa kubeba uzito wa tani 63 kila moja kwa wakati.
  • Mashua elekezi (Tugs) zinazowezesha meli kubaki katika njia yake wakati wa kutia nanga
  • Matishari yenye uwezo wa kubeba uzito wa tani 3,500 kila moja
  • Cargo Lighter yenye uwezo wa kubeba uzito wa tani 600
  • Pantuni za kuhamishia shehena
  • Mtambo wa kuhamishia makasha yasiyokuwa na kitu wenye uwezo wa kubeba uzito wa tani 12
  • Mitambo ya kubeba makasha yenye uzito wa tani 40
  • Matrekta (TT) ya kusaidia kuhamisha mizigo
  • Foko maalumu kwa kuhudumia marobota ya katani
  • Foko za kawaida saba
  • Foko nne zenye uwezo wa kubeba tani nne kila moja
  • Foko tatu zenye uwezo wa kubeba tani tano kila moja
  • Matela ya kuhudumia mzigo bandarini
  • Magari ya zimamoto yenye vifaa vya kukabiliana na moto
  • Boti ya kusaidia uegeshaji (Mooring Boat)
  • Mizani kwa ajili ya upimaji wa mzigo
  • Midaki ya kukagua mizigo
  • Hoppers kwa ajili ya kuhudumia mzigo wa kichele
  • Grabs kwa ajili ya kuhudumia mzigo wa kichele
 

Hifadhi

Bandari ya Tanga ina maghala matatu yaliyoezekwa kwa ajili ya shehena zinazoathiriwa na hali ya hewa.

  • Eneo lenye sakafu ngumu kwa ajili ya kuhifadhia makasha na shehena nyingine zisizohitaji kufunikwa lenye meta za mraba 29,000.
  • Maghala yaliyoezekwa yenye eneo la meta za mraba 13,800
 

Uwezo

Uwezo wa sasa wa bandari ambao umeboreshwa umewezesha kuhudumia tani 1,201,000 za shehena kwa mwaka.

 

Uboreshaji Bandari ya Tanga

Maboresho yanaendelea kwenye Bandari ya Tanga ikijumuisha kuongeza kina, kuimarisha gati namba moja na mbili na kuboresha uwezo wa kuhudumia meli na mzigo zaidi.

 

Kwa maelezo zaidi wasiliana na:

Meneja wa Bandari Tanga,
Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA),
Bandari House
S.L.P 443,
Tanga, Tanzania

Simu +255 (27) 2643078
Faski: +255 (27) 2642360
Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.