Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavara

Na Beatrice Jairo

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imezindua rasmi wiki ya huduma kwa mteja na kuvutia wadau mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo.

Wiki hiyo ambayo ilizinduliwa rasmi na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavara ilipambwa na rangi mbalimbali za Mamlaka ikiwa ni pamoja na kutoa zawadi mbalimbali kwa wateja.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhandisi Kijavara amesema maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja “Customer Service Week” yataongeza chachu ya kuhudumia wateja na kuongeza ufanisi.

Amesema kwamba, TPA inathamini mchango mkubwa wa wateja wake katika kusaidia kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato ambayo yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi kifupi.

Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi Mkuu, TPA imevuka malengo ya ukusanyaji wa mapato iliyojipangia.

Kwa upande wa wadau walioshuhudia uzinduzi huo, wameelezea kuridhishwa kwao na juhudi za uongozi wa Mamlaka hiyo kutafuta masoko na kuwafuata wateja walipo badala ya kuwasubiri ofisini.

Wamesema kwamba huo ndio mfumo mzuri na wa kisasa wa kutafuta masoko na kuboresha uhusiano ulipo na wateja.

  Mwisho