Na Leonard Magomba

Wafanyabiashara toka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), wamefanya ziara ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam ili kujionea miundombinu ya Bandari hiyo pamoja na kukagua maboresho mbalimbali yaliyokwishafanyika na yanayoendelea kufanyika.

DRC ambalo ndilo soko kuu kwa Bandari ya Dar es Salaam hutumia Bandari hiyo kupitisha bidhaa mbalimbali haswa za madini ya aina mbalimbali yanayopatikana nchini humo, sambamba na mazao ya misitu.

Kwa upande wa bidhaa zinazoingia kutoka katika soko la kimataifa, DRC inapitisha bidhaa za nafaka, magari, mitambo, mavazi, vinywaji, mafuta na bidhaa za chuma.  

Kabla ya ziara ya kutembelea miundombinu ya Bandari, wafanyabiashara hao walifanya mazungumzo katika ukumbi wa mikutano uliopo jingo la TPA Tower na menejimenti ya TPA chini ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Lufunyo Hussein.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Lufunyo aliwakaribisha na kuwashukuru kwa kuendelea kuiamini na kutumia Bandari za TPA hususani Dar es Salaam, Tanga na Kigoma kupitisha shehena mbalimbali zinazoingia na kutoka nchini DRC.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu alitumia fursa hiyo, kuwahakikishia usalama wa mizigo yao na utayari wa TPA kuendelea kutoa huduma bora na zenye ufanisi zaidi kwa wafanyabiashara hao kwa maslahi mapana ya nchi zote mbili.

Akifafanua kuhusu Ulinzi na Usalama, Dkt. Lufunyo aliwaeleza wafanyabiashara hao jinsi mifumo ya kisasa ya Ulinzi na Usalama inavyofanyakazi ambapo alisema TPA imefunga takribani Kamera 400 za CCTV kuzunguka eneo la Bandari nzima ambazo zinafanyakazi saa 24.

Akizungumza kwa niaba ya ujumbe wa wafanyabiashara hao kutoka nchini DRC katika miji ya Kalemie, Uvira, Bukavu na Goma, Mwenyekiti wa Umoja huo aliishukuru TPA kwa huduma bora zinazotolewa katika Bandari hiyo.

Mwenyekiti huyo alisema kwamba, kwasasa mizigo yao inahudumiwa kwa ufanisi na kuwafikia kwa wakati.

Pia alipongeza kuwa siku 30 huru zinazotolewa na TPA kwa wafanyabiashara wa DRC pasipo kutozwa tozo ya kuhifadhia mizigo (storage charges) imesaidia wafanyabiashara hao wa DRC wanaotumia Bandari hizo kupunguza gharama za kupitisha Shehena kwenda katika miji hiyo.

Mwenyekiti huyo, aliwahakikishia TPA kuwa wafanyabishara hao toka nchini DRC wapo tayari kuendelea kufanyabishara na Bandari za TPA kwani zimekuwa na unafuu mkubwa wa gharama na wenye faida mtambuka kwa pande zote ukilinganisha na Bandari shindani.

mwisho